
Mstaafu wetu wa kima cha chini cha mshahara anaomba kulirudia tena hili kwamba anapokea mshahara wa Sh115,000 kila mwezi, kwenye nchi hiihii ambayo wawakilishi wasemekanao kuwa ni wa wananchi kama yeye, walau katika hili la kupokea laki si pesa, hajasikia wakifungua midomo kumwakilisha. Wanapokea shilingi milioni…mama wee…16 kwa mwezi huohuo. Kweli, aliyeshiba hamjui mwenye njaa.
Cha ajabu, wako wengi wanaopaswa kumsemea mstaafu hili la kupata pensheni ya Laki si Pesa kwa mwezi, lakini kila mmoja ameuchuna. Ni kama vile nchi hii haina wastaafu wa kima cha chini ambao wanapokea Laki si Pesa kwa mwezi, kama sio wameishakwenda Burundi walikoshauriwa kikejeli na mheshimiwa mmoja waliyemsomesha bure kwa ‘Pay As You Earn’ yao, kwamba waende!
Wako wengi wanaopaswa kufungua midomo kumsemea huyu mstaafu wa kima cha chini anayepokea na kuishi kimiujiza kwa shilingi laki moja na elfu kumi na tano kwa mwezi, lakini kila mtu ameuchuna, mradi yeye anapata zinazomtosha, hao wastaafu wa kima cha chini watajiju wenyewe, potelea mbali kwamba wao ndio walioipa nchi hii uhuru wake, kuijenga kwa jasho na damu yao na kuanzisha kibubu cha kwanza kabisa cha akiba ya wafanyakazi, ambako sasa hela yao ni kama inatapanywa ovyo kwa watu, lakini siyo kwa mstaafu!
Kuna mawaziri, makatibu na wakurugenzi wastaafu ambao tulijenga nao nchi tukiwa pamoja na ambao bila shaka sasa wanapata pensheni inayoeleweka na inayopata nyongeza kila baada ya miaka miwili au mitatu, ili waweze kukabiliana na hali ngumu ya maisha.
Ni ajabu sana kwamba na wao sasa wametusahau wastaafu wenzao kiasi kwamba hata kufungua tu mdomo kutusemea kwamba tunahitaji nyongeza ya pensheni, wako kimyaa kama vile kuna anayewataka wasizungumze chochote kuhusu suala la wastaafu wa kima cha chini asilani. Kweli, aliyeshiba hamjui mwenye njaa!
Kuna hivi vyama vya upinzani, vinavyopaswa kuitwa tu vyama mbadala, viko kimyaa kama vile nchi hii haina wazee wanaostahili kusemewa. Inaelekea havina sera yoyote ya kuwatunza na kuwasemea wazee wa nchi hii zaidi ya kutuhimiza tu wastaafu tuamke asubuhi siku ya uchaguzi kwenda kuwapigia kura! Kura zetu mnazitaka lakini hali zetu hamzitaki wala kuzizungumzia! Mabadiliko angalau yaanzie hapa pa kuwasemea wastaafu wa kima cha chini.
Hapa pa wachungaji na mashehe wa dini zetu kubwa mbili tumeshasema na kuomba kwamba sisi ni waumini wao wanaopaswa kufungua midomo yao na kupaza sauti kutusemea. Wastaafu wana uhakika kwamba viongozi wao wa kidini pia hawawezi kuishi kwa shilingi laki moja na elfu kumi na tano kwa mwezi,
Mbona wanataka sisi waumini wao wazee tuishi kimiujiza kwa ‘laki si pesa’ kwa mwezi, wakati miujiza ilibaki enzi zilee za mikate mitano na samaki wawili kwa maelfu ya waumini? Kemeeni hili, ili sisi waumini wenu tuongezwe pensheni! Hatuwezi kuishi kwa miujiza karne hii. Miaka 21 ya kutaka, na kukosa, nyongeza ya pensheni imetosha. Wastaafu wa kima cha chini sasa tumechoka kuishi kimiujiza.
Halafu kuna hawa wasemekanao kuwa ni wanaharakati wa haki za binadamu, sijui zipi lakini inaelekea sio za mstaafu wa kima cha chini.
Hivi mnayo habari kweli kwamba mstaafu wa kima cha chini wa nchi hii anapokea pensheni ya shilingi laki moja na elfu kumi na tano kwa mwezi wakati mwakilishi wake anayepaswa kumsemea lakini hafanyi hivyo, anapokea mamilioni ya shilingi mwezi huohuo? Mbona hampiganii haki yake ya kustahili kugawiwa keki ya taifa, wakati yeye ndio aliwasha jiko ili kuipika? Mbona mmeuchuna kuhusu hili?
Wote hawa tunawataka wafungue vinywa vyao kulikemea hili. Waanze na Siri-kali yenyewe. Mwezi Oktoba mwaka jana Siri-kali ilitangaza kwa mbwembwe kwamba ilikuwa inamuongeza mstaafu wa kima cha chini shilingi alfu hamsini, rudia hapo, alfu hamsini ili apate pensheni ya shilingi laki moja na elfu hamsini kumwezesha kukabiliana na hali ngumu ya maisha inayomkabili. Tukafarijika, japo shilingi elfu hamsini isingetuwezesha, isingemwezesha yeyote, kukabiliana na hali ngumu ya maisha.
Siri-kali ikaharibu. Ikatangaza kuwa nyongeza hiyo itapatikana baada ya miezi mitatu, kuanzia Januari. Hawakutoa sababu yoyote ya kufanya hivyo. Kwa kuwa mstaafu wetu alishaumwa na nyoka mara nyingi tu na anapoona jani hakawii kushituka! ‘Jani’ la Siri-kali likamshiitua. Kwa nini isubiri miezi mitatu ndio iwape wastaafu wake nyongeza ya pensheni? Si wangesubiri tu mwezi Januari wakatangaza nyongeza na kuwapa mwezi huohuo? Nikaishia kuwaambia wastaafu wenzangu wakae chonjo, saa mbaya! Siri-kali ilikuwa inataka kuonekana inaupiga mwingi kwa wastaafu baada ya miaka 21.
Mwezi Januari ukafika na kupita. Hakuna nyongeza ya elfu hamsini wala nini kwa mstaafu. Aliyepata sana amepata elfu kumi tu wengine alfu tano, sita au saba. Na wahusika wameuchuna tu hakuna maelezo yoyote. Mstaafu wa miaka 70 mpaka 80 unampa nyongeza ya shilingi alfu hamsini halafu unaiingiza kwenye kikotoo wakati wastaafu wa kima cha chini wote wapo kima cha chini na hakuna madaraja? Au urefu wa kamba waliyoruhusiwa waheshimiwa imefika mpaka kwenye pensheni ya wastaafu?
Siri-kali inataka sasa mpaka wastaafu wavue mashati na magauni na uzee wao wakalale kwenye geti la kuingilia Ikulu ili Rais ajue kuwa nyongeza ya wastaafu imechikichiwa. Aibu itakuwa ya nani? Wapeni wastaafu elfu hamsini yao, kama sio laki tatu kwa mwezi yao! Wastaafu wenyewe wa kima cha chini wamebaki wangapi ndugu zangu?
0754 340606 / 0784 340606