KONA YA MZAZI: Asemaye mtoto amenishinda ni mzazi mzembe

Bibi yangu aliwahi kuniambia kazi ya kumjengea mtoto maadili ni sawa na kazi ya mfinyanzi anayetengeneza vyungu bora kwa matumizi mbalimbali.

Kuna wafinyanzi wanaoipa thamani kazi yao, hivyo bidhaa zao huvutia wateja. Lakini wapo pia wanaofinyanga bila uangalifu na bidhaa zao hukosa mvuto au ubora hata kwa macho yao wenyewe baada ya kuziweka sokoni.

Ndivyo ilivyo kazi ya malezi, ni sanaa inayohitaji umakini, utulivu na kujitoa kwa dhati. Katika dunia ya sasa, watoto hukumbana na aina nyingi za malezi kutoka kwa watu tofauti tofauti.

Mzazi akiwa mzembe au mwenye upungufu wa uangalizi, huenda akajikuta mtoto wake akitumbukia kwenye janga la malezi mabaya.

Ndiyo maana leo hii si ajabu kusikia mzazi akisema: “Mtoto huyu amenishinda” au “Nimekata tamaa, siwezi tena.” Lakini swali ni hili: kama si wewe mzazi wake wa kumzaa, ni nani atakayemwelekeza njia sahihi?

Kumbuka, mwalimu wa kwanza wa mtoto ni mzazi. Unachokipanda leo katika akili na moyo wake, hata kama hujakusudia, ndicho utakachovuna kesho.

Ukishindwa kumpa maarifa, maadili na mwongozo wa maisha, dunia haitakosea nafasi ya kumfundisha, lakini si lazima iwe kwa njia njema.

Usidanganyike kuwa kimya chako kinamaanisha mtoto hajui kitu. Wanaweza kuwa wanajifunza kutoka kwa mitandao, marafiki au vyanzo visivyo sahihi.

Maadili ya kweli huanzia nyumbani na huwa na mizizi mirefu kuliko yale yatolewayo na dunia ya nje.

Tukubaliane, kulea mtoto si kazi rahisi. Ni jukumu linalopaswa kushirikisha familia nzima, lakini mzazi ndiye dereva wa safari hiyo.

Usijivike taji la mzazi bora kama hujui kinachoendelea katika maisha ya mtoto wako kwa sababu unakimbizana na shilingi mchana kutwa. Dunia ikimlea mwanao, usishangae matokeo.

Kila mzazi humtarajia mtoto wake afanikiwe. Lakini matarajio hayo hayawezi kutimia bila kujitoa mapema.

Watoto wote wamejaliwa vipaji, lakini vipaji hivyo vinahitaji kupaliliwa kwa malezi mema. Unaweza kumpa mwanao elimu bora, lakini bila msingi wa maadili na usimamizi, ndoto zako kwake zitayeyuka.

Ni kweli mazingira yamebadilika na majukumu yameongezeka. Lakini hali hiyo isiwe sababu ya kuzembea. Jipangie ratiba ya kuhakikisha unakuwa karibu na watoto wako.

Hata kama huna muda wa kutosha, tafuta angalau nyakati muhimu kama wakati wa chakula cha jioni au kifungua kinywa, kuzungumza nao.

Mazungumzo hayo hata ya kawaida tu kuhusu siku yao yalivyokuwa, hujenga ukaribu na hufungua milango ya watoto kusema yanayowasumbua. Hapo ndipo upendo wa kweli hukua, na urafiki baina ya mzazi na mtoto huimarika.

Kwa bahati mbaya, tafiti zinaonesha kuwa wazazi wa kiume barani Afrika hupata nafasi chache kuwa na familia zao nyakati za jioni. Lakini ukiweka kipaumbele, unaweza kubadilisha hali hiyo.

Kazi ya familia kushiriki pamoja nyakati za sherehe kama Iddi, Krismasi, Pasaka au hata sikukuu za kitaifa. Safirini pamoja au fanyeni shughuli za kifamilia kwa pamoja.

Mkaribishe rafiki wa mtoto wako nyumbani, waruhusu watoke lakini kwa uangalizi. Hayo ni mambo madogo lakini yenye athari kubwa katika maisha ya mtoto.

Usisubiri mpaka mtoto apate matatizo ndipo ujue thamani ya malezi. Kama alivyosema bibi yangu: “Mzazi ni kama mfinyanzi, kazi yake inaonekana katika ubora wa chungu alichokiumba.”

Simama kwenye nafasi yako ya mzazi, wajibika, zungumza, elekeza na kuwa karibu na muhimu zaidi, kuwa rafiki wa kweli wa mtoto wako.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *