KONA YA MSTAAFU: Kibubu cha wastaafu kinavyoiga jamii katika utendaji wake

Mstaafu wetu anakitazama kibubu ambacho kimemtunzia hela yake na ya wastaafu wenzake kwa miaka 40 aliyokuwa mwajiriwa, na anajikuta akisikitika sana kuona jinsi sasa kinavyofanya kazi zake kwa namna inayofanana na jamii yetu ambayo hayamsaidii sana mstaafu, bali inamuumiza zaidi pamoja na kwamba hela zake ndizo zilitumika kukianzisha na kukijenga kibubu hicho.

Yapo mengi ambayo mstaafu wetu anaona kama kibubu kinayachukua kutoka kwa jamii na kuyafanya ndiyo utendaji kazi wake, eti kwa faida ya mstaafu.

 Leo anaomba azungumzie hili moja ambalo kibubu kinadhani kimemsaidia sana mstaafu kumbe hakimsaidii lolote kama jamii isivyomsaidia, lakini mwishowe inataka ionekane inafanya hivyo ili kujijazia maujiko, kama kinavyotaka kufanya Kibubu sasa!

Kuna hili la mstaafu anapougua maradhi yake ya kiutu uzima yanayoshika kasi sana anapostaafu. Kama mnavyojua, yale matibabu ya bure kwa wazee wa miaka 60 na zaidi yameishia kuwa maneno ya kanga tu, na mambo ya bima ya afya yanamlazimu mstaafu asumbue watoto wake ambao wengi bado wanaitafuta ajira kwa tochi au wanalazimika kusoma kwanza Veta na vidigrii vyao. Mwe!

Haya ni yale magonjwa ya kiutu uzima yasiyoambukiza lakini yanayomwandama mstaafu, kama kisukari, ugonjwa ambao mstaafu wetu huishia kujiuliza kwa nini tuuite kisukari wakati hauna utamu wowote bali ni machungu tu!

Ama ule wa kiharusi, ambapo mstaafu wetu anajiuliza kwa nini ugonjwa mkubwa huo wa watu wazima unaitwa kiharusi, wakati baada ya miaka 60 hakuna mstaafu atakayejisumbua kufunga kiharusi na kamchepuko kake.

Badala ya kuuita ugonjwa huo mbaya kiharusi, bora tuseme tu stroke, au kisambaa kwa msisitizo, kama Kiswahili hakina neno linalofaa kuuita ugonjwa huo!

Maradhi yanamkaba mstaafu wetu kisawasawa huku misaada kutoka kwa ndugu, jamaa, na marafiki ikipungua kadri umri wake unavyoendelea kustaafu.

Kwa hakika, inafikia mahali hospitali inamwambia mstaafu ili apone maradhi yake ni lazima apate dawa fulani, matunda, na lishe bora. Vitoke wapi sasa kwa pensheni ya shilingi laki moja na elfu kumi na tano kwa mwezi, huku matibabu yasiyokuwa ya bure hata kwa wazee wa taifwa miaka 60 na kuendelea?

Mungu alitoa na Mungu akatwaa. Mstaafu anarudi mavumbini alikotoka. Shangaa sasa! Wale ndugu, jamaa, na marafiki waliochoka na kuamua kukata kamba ya kutoa msaada, wanakanyagana ili kumsaidia mstaafu kurudi vyema mavumbini!

Mstaafu hakumbuki mara ya mwisho kuvaa suti tangu alipostaafu, lakini siku ile ya kupelekwa Kinondoni, suti na tai ziko kibwena tena mpya, si mitumba!

Wale ndugu, jamaa, na marafiki waliokata kamba na kuingia mitini badala ya kumpa lishe borana dawa ili aendelee kuishi, lakini wakauchuna, leo wanamnunulia maua ya bei mbaya wakati anarudishwa mavumbini! Ni wazi kuwa yale maneno ya wachungaji na masheikh wetu kuhusu kuwasaidia wagonjwa yanaingilia sikio hili na kutokea lile! Mstaafu anashangaa kuona kibubu cha akiba ya wastaafu kama kimeiiga jamii sasa, kikitaka kionekane kimemsaidia sana mstaafu kumbe si lolote.

Kibubu hiki, ambacho hakijawahi kumpa mstaafu hata huduma ya mkopo au kumuongezea chochote kwenye pensheni yake, pamoja na kukaa na hela zake kwa miaka 40 ya ajira yake!

Kibubu kimetangaza kuwa siku mstaafu anaporudi mavumbini, kwanza kitatoa shilingi laki tano (hapa tusisahau kwamba pensheni ni shilingi laki moja na elfu kumi na tano kwa mwezi!) kama msaada kwa vitegemezi vyake wa kumpeleka Kinondoni.

Kisha, kitatoa shilingi milioni tano kwa vitegemezi hivyo ili wamudu maisha yao wakati mstaafu atakuwa amerudi mavumbini. Kibubu kimezitangaza ofa hizi mbili kubwa kwa wastaafu watakaorudi mavumbini kuanzia mwaka 2024.

Sawa, ni jambo jema, lakini mstaafu angependa kujua zaidi: je, wale wastaafu wenzake ambao walisharudi mavumbini tangu mwaka 2020 na nyuma zaidi, vitegemezi vyao vimeitwa kupata hizo laki tano na hizo milioni tano zilizotangazwa, au ndiyo imetoka hiyo, ikirudi pancha, wakati hela zao bado zilikuwepo kibubuni na zikifanyiwa biashara?

Je, kibubu kinahakikishaje kitawapa vitegemezi wa mstaafu hizo laki tano na milioni tano, wakati hakijawahi kumpa mstaafu hata nyongeza ya pensheni, kumuandalia bima ya afya, au hata kumkopesha pamoja na kwamba hela yake ipo Kibubuni na inaweza kumdhamini?

Anachoona mstaafu ni yale yale ya ndugu, jamaa na marafiki—kutaka kuonekana wanamsaidia sana anaporejea mavumbini, si anapohangaika kuishi!

Mstaafu ana wazo: hizo milioni tano na laki tano apewe akiwa hai, ajue mwenyewe na wategemezi wake cha kufanya kabla ya kurudi mavumbini. Si zake? Ikiwa kimeshindwa hata kumkopesha au kumnunulia bima ya afya, si anaweza kujitokeza mtu na kusema vitegemezi wachape lapa maana hakuna milioni tano hapo? Inawezekana! Nyongeza ya pensheni imeishia wapi?

Mpeni mstaafu milioni tano yake akiwa hai. Msingoje mpaka akirudi mavumbini! Kama hamkuweza kumpa mkopo kwa miaka 25 ya ustaafu wake mkiwa na hela zake, mtaweza kuwapa vitegemezi wake milioni tano akiwa mavumbini? Mna tofauti gani na jamii inayolaumiwa hata kwenye ibada?

 0754 340606 / 0784 340606

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *