
Watanzania 16 wamepoteza maisha Kariakoo, Dar es Salaam. Familia nyingi zimebubujikwa machozi baada ya kuondokewa na ndugu zao waliowapenda na waliogusa maisha yao kwa namna mbalimbali.
Matumaini ni jinsi Jeshi la Wananchi Tanzania (JWTZ), lilivyoingia kazini kuokoa watu waliokwama chini, baada ya kufunikwa na jengo lililoanguka. Jeshi ni fahari ya nchi. Nyakati zenye uhitaji kama Kariakoo, wanaume waliovalia sare wanapofika kufanya uokoaji, wananchi hutazama kwa kujivuna; jeshi letu!
Ndoto ya Tanzania bado ipo hai. Vijana wasio na mafunzo ya uokoaji, waliwiwa kufanya kitu ili kuokoa ndugu zao waliokwama ndani ya jengo lililoanguka Kariakoo. Ndoto ya Tanzania ni mbegu iliyopandwa na waasisi wa Jamhuri. Mbegu ya hamasa na mguso wa moyo wa kujitoa. Usitazame, fanya kitu kwa ajili ya mwenzako. Fanya kitu kwa ajili ya nchi yako.
Wiki ya tafakuri ya ujenzi holela unavyogharimu maisha ya watu na uchumi. Serikali ilibidi ijielekeze Kariakoo kusimamia uokoaji. Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa, mtendaji mkuu wa Serikali, lakini alisimamisha kila kitu kwa ajili ya Kariakoo. Jumlisha mawaziri wengine na Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Albert Chalamila.
Ni tafakuri kuhusu Tanzania. Mamlaka hushituka maafa yanapotokea. Husimama kidete na kutoa kauli zenye matumaini. Kamati huundwa kufanya uchunguzi. Ripoti hutoka. Mambo yakipoa kila kitu husahaulika. Hii ndiyo sababu ujenzi wa maghorofa ni hatari Tanzania.
Kuanzia Hoteli ya Chang’ombe Inn iliyoporomoka Keko, Dar es Salaam mwaka 2006, hadi jengo la ghorofa 16, lililoanguka mtaa wa Indira Ghandi, Dar es Salaam, Machi 2013 na kuua makumi ya Watanzania. Majengo kuendelea kuanguka ni kielelezo cha mamlaka kutochukua hatua stahiki baada ya ajali za nyuma.
Desemba 2021, jengo la ghorofa lilianguka Goba, Dar es Salaam, likaangukia nyumba yenye wakazi, likasababisha vifo vya watu wanne na majeruhi 17. Mwaka 2008, ghorofa lilidondoka Kisutu, Dar es Salaam. Februari 2013, ghorofa lilidondoka Kijitonyama, Dar es Salaam na kusababisha kifo cha mtoto aliyekuwa na umri wa miaka tisa.
Ongeza majengo mengine yote ya ghorofa yaliyoanguka, hasa Dar es Salaam. Kila ajali, matamko hufuata, kamati huundwa. Mwaka 2006, baada ya ajali ya Hoteli ya Chang’ombe Inn, aliyekuwa Waziri Mkuu, Edward Lowassa, aliunda kamati. Ripoti ilitoka. Ikaonesha Dar es Salaam, hasa Kariakoo kuna utitiri wa majengo yaliyojengwa chini ya kiwango.
Naikumbuka kauli ya Waziri Mkuu baada ya Lowassa, Mizengo Pinda bungeni, kuhusu ujenzi chini ya kiwango Dar es Salaam. Usingetarajia mpaka sasa watu waendelee kupandisha maghorofa yenye kuhatarisha maisha ya wengine. Ghorofa linajengwa, linapanda juu, kisha linasababisha mauaji, mamlaka zipo. Serikali za mitaa zipo.
Maumivu Kariakoo yapo kuanzia majeruhi mpaka waliopoteza mali zao katika ajali. Vijana wa Kitanzania wanahangaika kujenga na kukuza mitaji. Wanapanga kwenye jengo la biashara. Wakiwa wamefika mahali wakijiona tayari wameshapata ukombozi wa kimaisha, wanakutana na dhoruba kali. Wamerudi nyuma.
Uzembe wa kutochukua hatua stahiki haraka, unasababishia vijana wa Kitanzania umaskini. Laiti mwenyekiti wa serikali ya mtaa angetimiza wajibu wake. Mjumbe wa eneo husika angewajibika. Mamlaka za utoaji vibali vya ujenzi na ukaguzi wa majengo, zote zingefanya kazi zao kwa umakini, leo kusingekuwa na mjadala wa jengo Kariakoo kuanguka na kusababisha maafa, majeruhi na upotevu wa mali.
Ni tafakuri kuhusu mfariji mkuu wa nchi, Rais Samia Suluhu Hassan. Kupanda ndege kuelekea Brazil kwenye mkutano wa G20, Watanzania wenye kuhitaji faraja yake wakiwa wamefunikwa ndani ya ghorofa lililoanguka. Makumi wakiwa hawajui hatima yao.
Mkutano wa G20 ni muhimu sana. Pamoja na hivyo, maisha ya Watanzania ni muhimu zaidi. Uamuzi wa kuahirisha ziara ya Brazil, lingekuwa tendo la faraja kwa Watanzania. Hii inahusu pia washauri wa Rais. Lazima wahakikishe wanaunda vipaumbele vya mahali Rais anapopaswa kwenda.
Yupo mtu anaweza kusema Rais Samia angebaki ndiye angekwenda Kariakoo kuokoa watu? Mwingine atahoji mbona Waziri Mkuu amesimamia suala la Kariakoo tena kwa maagizo ya Rais? Naweza kuwauliza; nchi imefikwa na maafa. Viongozi wa nchi nyingine wakitaka kumpa pole, wanampa akiwa Brazil au Tanzania?
Unasafiri wakati nyumbani kwako kuna msiba. Unataka majirani na jamaa wa mbali wakupigie simu ukiwa safarini wakupe salamu za pole. Bila shaka, inapendeza Rais Samia angebaki Tanzania. Mikutano ya G20 ipo. Fursa zake haziwezi kulingana na maisha ya Watanzania anaowaongoza.
Katikati ya msiba Kariakoo, kuna maigizo yakafanyika Arusha. Mkuu wa Mkoa, Paul Makonda, alikusanya wanahabari kwenye ukumbi wa Kituo cha Kimataifa cha Mikutano Arusha (AICC). Agenda ni kutoa ripoti ya ufanisi wake ndani ya miezi sita tangu alipoteuliwa na kuapishwa kuongoza mkoa huo.
Arusha ina wanahabari wa kutosha. Makonda alikusanya wanahabari kutoka Dar es Salaam. Je, nani alilipa gharama zote hizo? Vyombo vya habari vinavyolia hali ngumu ya kiuchumi, ndivyo vilisafirisha wafanyakazi wao kwa sababu Makonda kutimiza miezi sita Arusha ni jambo kubwa?
Kama Makonda ndiye aliyebeba gharama, pesa alitoa wapi? Mkoa wa Arusha una bajeti kubwa kuliko mikoa mingine? Makonda alipokuwa Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, alikuwa akimwaga fedha kuliko wakuu wa mikoa wengine wote. Niliwahi kuandika makala nikiuliza; Makonda ni mjanja sana au ana moyo mkarimu kuliko wakuu wengine wa mikoa?
Maigizo ya mkutano huo ni kuwa badala ya agenda ya miezi sita Arusha, sehemu kubwa aliitumia kujisafisha kwa kashfa mbalimbali zinazomkabili. Tukio lake la kuvamia ofisi za Clouds Media Group (CMG) na mitutu ya bunduki mwaka 2017, tuhuma za kuhusika na shambulio la risasi dhidi ya Makamu Mwenyekiti wa Chadema, Tanzania Bara, Tundu Lissu, vilevile kupigwa marufuku kukanyaga Marekani.
Wiki ijayo nitaandika zaidi kuhusu Makonda na mkutano wake wa miezi sita.