
Desemba 10, 2024, Chadema walipotangaza kwa mara ya kwanza msimamo wao wa “No Reforms No Election” – “Bila mabadiliko ya Katiba kwenye mfumo wa uchaguzi hakutakuwa na uchaguzi”, ni wakati ambao Romania, wao uchaguzi wa kumpata rais wao ulikuwa umefutwa.
Romania, kilichosababisha uchaguzi ufutwe ni dola. Idara za usalama za nchi hiyo, zilidai kunusa harufu ya taifa lao kuingiliwa. Kwamba, nchi hiyo ya Ulaya Mashariki, yenye uanachama wa Jeshi la Kujihami la Nchi za Magharibi (Nato), ilikaribia kuwekewa Rais na Russia.
Tuhuma ni kuwa aliyekuwa mgombea binafsi, Calin Georgescu, hakuwa mwanasiasa tishio. Kipindi cha kampeni, ghafla mitandao ilishika agenda ya kumuunga mkono. Kisha akaongoza duru ya kwanza ya uchaguzi, kinyume na matarajio ya wengi. Aliyeshika nafasi ya pili ni mwanahabari mashuhuri aliyegeukia siasa, Elena Lasconi.
Georgescu aliongoza lakini hakupata kura asilimia 50 jumlisha moja, inayotakiwa kikatiba. Ilibidi mchuano urudiwe wa wawili; Georgescu dhidi ya Lasconi. Zilibaki saa 48 Waromania wapige kura ngwe ya pili kumpata rais wao mpya, ambaye angemrithi Rais Klaus Iohannis, ambaye aliachia ngazi Februari 12, 2025. Hivi sasa, Romania wanaongozwa na Rais wa Mpito, Ilie Bolojan, ambaye kabla alikuwa Rais wa Baraza la Seneti la Romania.
Uchaguzi wa Romania ulizuiwa na mahakama. Idara za usalama baada ya kukusanya ushahidi kuhusu nchi hiyo kuvamiwa na Urusi, ziliwasilisha shauri mahakamani kuzuia uchaguzi. Walibaini kuwa akaunti nyingi za mitandao ya kijamii, ambazo awali zilifunguliwa kwa malengo tofauti, ghafla ziligeuka majukwaa ya kisiasa, tena zikilipiwa fedha nyingi za matangazo ili kumuunga mkono Georgescu. Akaunti hizo, ziliongozwa kutokea nje ya Romania.
Tutazame hilo; uchaguzi Romania ulizuiwa na dola. Rais Iohannis na mifumo walitaka. Ni rahisi walio upande wa dola kufanikisha kufutwa, kuzuiwa au kuitisha uchaguzi wa marudio, kuliko wapinzani. Romania ni mfano. Zanzibar ilishatokea katika sinema ya Jecha Salim Jecha Oktoba 2015. Angola nyakati za Jonas Savimbi.
Kenya, Uchaguzi wa Rais 2017, ulibatilishwa na mahakama. Malawi pia, Uchaguzi wa Rais 2019 ulitenguliwa na mahakama. Hapa ni kujenga hoja kuwa hata bila utashi wa dola, inawezekana kuzuia uchaguzi kupitia mahakama. Swali, je, mfumo wa kimahakama Tanzania upo kwenye nafasi ya kubariki No Reforms No Election? Kisha, mahakama izuie uchaguzi usifanyike 2025?
Tunarudi tulipoanzia; Chadema walitambulisha kwa mara ya kwanza msimamo wa No Reforms No Election, Desemba 10, 2024. Siku mbili baadaye, yaani Desemba 12, 2024, chama hicho kikaanza safari ya mgawanyiko. Siku wanatangaza No Reforms No Election kama tamko la Mkutano Mkuu wa chama hicho, Mwenyekiti wa sasa, Tundu Lissu, na mtangulizi wake, Freeman Mbowe, walikuwa kitu kimoja.
Siku mbili baadaye, wakaanza kuvuana nguo. Chama kikapasuka kuelekea uchaguzi mkuu wake, uliofanyika Januari 21, 2025. Zaidi ya siku 50, Chadema waliondoka kwenye msimamo wao, wakaanza kushughulikiana wao kwa wao. Hii ni Machi 2025, ndiyo Lissu anakusanya nguvu ili aanze kampeni ya No Reforms No Election.
Juni 2025, Bunge la Tanzania linatarajiwa kukoma muhula wake wa miaka mitano. Hakuna mabadiliko ya Katiba, hata yawe madogo kiasi gani, wala utunzi wa sheria yoyote, unaoweza kufanyika bila Bunge. No Reforms No Election, inaweza kuliwahi Bunge kabla halijavunjwa? Sayansi gani inatarajiwa kutumika?
No Reforms No Election, ilianza kupoteza mguso wake, siku Lissu alipoanzisha mapambano dhidi ya Mbowe. Hivi sasa, chama hakijawa kimoja. Kuna misuguano ya ndani kwa ndani. Machi 8, 2025, Lissu alikuwa anawakabili wanaomwita dikteta ndani ya Chadema. Alikuwa akiwajibu wanaosema No Reforms No Election ni msimamo wake binafsi. Hili lilikuwa kuonesha kuwa chama bado kina mgawanyiko.
Laiti, Chadema wangebaki wamoja baada ya tamko lao siku ya kwanza, pengine kufikia sasa wangeshakuwa wamepiga hatua nyingi mbele. Walichagua kuparurana wao kwa wao ndani kwanza. Hivi sasa wanahitaji muda wa kuendelea kupona. Wakati huohuo, muda haupo upande wao.
Pengine, kuna matarajio ya kuitisha Bunge la dharura kwa ajili ya kufanya mabadiliko madogo ya Katiba na kutunga sheria. Anayepaswa kuitisha hilo Bunge ni Rais Samia Suluhu Hassan. Je, ana utashi huo? Vipi, bajeti ya kulihudumia hilo bunge hata kama litaketi wiki moja itapatikanaje? Utayari wa kulihudumia utakuwepo?
Sayansi ya siasa inaelekeza njia hiyo ya kupitia Bunge, vilevile kuuangukia umma, utoe presha kwa Serikali ili Rais Samia aone kuna ulazima. Je, msuli wa kuushawishi umma upo? Hivi karibuni, baada ya wito na matangazo mengi, hatimaye Chadema walitangaza kupokea michango Sh64 milioni. Fedha hizo siyo tu hazitoshi kuzunguka Tanzania kuhamasisha umma, bali pia ni kipimo cha kushuka kwa ushawishi.
Mwaka 2020, Chadema waliweza kuchangisha zaidi ya Sh300 milioni kwa siku mbili, kulipia faini viongozi wa kitaifa wa chama hicho, waliokutwa na hatia mahakamani. Februari 2025, kwa zaidi ya wiki mbili, fedha zilizopatikana ni Sh64 milioni. Kwa namna hii ya kushuka kwa ushawishi, sayansi ipi itatumika kutia presha uchaguzi usifanyike mpaka kuwepo mabadiliko? Au No Reforms No Election ni mwanzo wa utani mkubwa kisiasa?