
Mguu uliomwingiza Tundu Lissu kwenye hatamu Chadema, ndiyo uliomwondoa Freeman Mbowe. Mdomo uliopukutisha imani ya wana-Chadema kwa Mbowe, ndiyo uliomsafishia njia Lissu.
Waingereza wana methali isemayo: “Give a dog a bad name and hang him.” – “Mpe mbwa jina baya na umnyonge.” Ikiwa na maana kuwa ukishamwondolea mtu heshima yake kwenye jamii, utayafanya maisha yake kuwa magumu.
Mfanano wake ni methali: “He that has an ill name is half hanged.” – “Ambaye ana jina baya ni nusu ya aliyenyongwa.” Lissu aliingia kwenye kiti kwa kumpa Mbowe jina baya. Heshima ya Mbowe iliyeyuka.
Thiolojia ya Kikristo inafundisha kuhusu dhambi ya asili (original sin). Kwamba ni ile ambayo binadamu wameirithi kutoka kwa wazazi wakuu wa ulimwengu; Adam na Hawa. Kwa mujibu wa mafundisho hayo, dhambi ya asili inamgusa kila binadamu.
Utoaji wa jina baya na kunyonga ni dhambi ya asili Chadema. Zitto Kabwe, alipewa jina baya kuwa ni msaliti, aliyenunuliwa ili kuivuruga Chadema. Zitto alikwenda kuanzisha ACT-Wazalendo akiwa “ameshanyongwa”. Mpaka leo maumivu hayajapona.
Dk Willibrod Slaa, alikuwa Pilato, aliyeongoza ugongaji misumari kwenye msalaba uliomning’iniza Zitto. Muda ulipofika, Slaa naye alipewa jina baya. Aliambiwa amenunuliwa na CCM ili ahujumu Chadema kwenye Uchaguzi Mkuu 2015.
Slaa, alijaribu naye kuwapa majina mabaya viongozi wa Chadema waliobaki kupitia kitabu chake, “Nyuma ya Pazia”, lakini hakuweza kuwanyonga. Ni dhambi ya asili Chadema. Frederick Sumaye, aliitwa kibaraka, kama ilivyo kwa Profesa Kitila Mkumbo, Profesa Abdallah Safari na wengine.
Marehemu Chacha Wangwe, naye alipewa jina baya. Kwamba eti alikuwa akitumiwa na CCM kuihujumu Chadema. Akasimamishwa uongozi wa chama. Mauti yalimkuta Wangwe akipigania kujitoa kwenye kitanzi kilichokuwa kinamning’iniza.
Dhambi asilia ya Chadema ni kutokuheshimu dhana ya kutofautiana jinsi ya kuwaza na ujengaji hoja. Yeyote mwenye mawazo tofauti, namna yake ya kumshughulikia ni kumnadi kwamba amehongwa na CCM, kisha wanachama humshughulikia.
Mbowe baada ya kunufaika kwa muda mrefu na dhambi hiyo, ikamgeuka. Lissu alikuwa mkono wa kulia wa Mbowe kwa muda mrefu. Bila shaka aliijua falsafa. Akamtandika mfululizo kwa kumpa majina mabaya. Mbowe akaanguka chali. Lissu ndiye Mwenyekiti leo.
Asili na historia, kotekote inaonesha kwamba Chadema huwezi kuwa na mtazamo tofauti au mawazo yenye kukinzana na uongozi kama hujahongwa. Msimamo wowote utakaouchukua au kuuonesha, kinyume na chama, wewe unakuwa kibaraka wa CCM.
Halima Mdee na wenzake 18, walipokula kiapo kuwa wabunge wa viti maalumu, kinyume na msimamo wa chama, moja kwa moja walipewa jina baya. Hivi sasa, Halima na wenzake ni sawa na mtu aliyenyongwa nusu.
Ndani ya Chadema limeibuka kundi jipya, linaitwa G55. Wao wanapinga utekelezaji wa msimamo wa chama wa “No Reforms, No Election.” – “Bila mabadiliko ya sheria, mifumo na kanuni za uchaguzi, hakuna uchaguzi.” G55 wanataka chama kiingie kwenye uchaguzi.
G55 wanatilia shaka uwezo wa chama hicho kizuia uchaguzi, na wanasema haitawezekana chama hicho kufanya Uchaguzi Mkuu 2025 usifanyike. Wanaonya hatari ya chama kutenda jinai, kukosa ruzuku na hata kupotea kabisa.
Kutoka hoja za G55, nimemsikia Lissu akiwaita “wajinga”. Mjumbe wa Kamati Kuu Chadema, Godbless Lema, aliandika kwenye akaunti yake ya X kuwa nyuma ya G55 kuna watu wanatengeneza fedha kutoka CCM. Hadithi ni ileile, hakuna kutofautiana mawazo hadi uwe umenunuliwa na CCM.
Dhambi ya asili Chadema, inagusa tabia ya kuukataa ukweli. Chama kimekuwa kikubwa, haishangazi kuibuka misuguano ya mawazo. Kukimbilia kushutumiana na kupakazana matope ni kujidanganya tatizo halipo. Hutaweza kulitatua.
Mwanafalsafa wa Uingereza, John Locke, kupitia kitabu chake “An Essay Concerning Human Understanding”, aliandika kwa ufafanuzi mpana kwamba binadamu ana kawaida ya kuzima fikra dhidi ya hitimisho asilolitaka.
Tamko la viongozi wakuu wa Chadema ni No Reforms, No Election. Msimamo huo unawafanya wazime fikra zao dhidi ya hoja yoyote ambayo inaweza kuwapa changamoto au kuwaelekeza kwenye hitimisho wasilolitamani.
Shida kuu ya G55 ni dhambi asilia. Timu ya Lissu, haitazami hoja za G55 kama zilivyo ili zijibiwe au kuwaita mezani kuzungumza kwa ajili ya kesho njema ya Chadema. G55 wanatazamwa kidogo, halafu kinatafutwa kivuli cha Mbowe.
Sababu ni uwepo wa imani kwamba Mbowe hajakubali kushindwa. Mmegombea, umemshinda uchaguzi. Amekubali matokeo. Akatoa ushauri wa kuponya majeraha. Kisha, amekwenda pembeni na kukaa zake kimya.
Majeraha hayajatibiwa. Anaibuka Lembrus Mchome, anahoji uhalali wa viongozi walioteuliwa na Lissu. Badala ya kujibiwa, anaambiwa katumwa na Mbowe. Wanatokeza G55, jina la Mbowe linatajwa tena. Je, ni mapambano dhidi ya kivuli, au kweli Mbowe hajakubali kukaa pembeni?
Ama Mbowe yupo nyuma ya G55 na Mchome, au uongozi wa Lissu unapambana na hofu isiyokuwepo, yote kwa yote ni matokeo ya kuruhusu siasa za kukanyagana. Vinyongo lazima viwepo. Wasiwasi hauwezi kuondoka haraka.
Unaweza vipi kutulia na kuongoza, wakati unatambua uliyemtoa kwenye kiti uliua wasifu wake? Tena mwenyewe awe amekaa kimya, hujui anachopanga au anayoyafikiria. Usipokuwa na hofu hata kidogo, basi utakuwa na shida kubwa ndani yako.
Kila kinachotokea Chadema, kwa kutazama historia, jinsi utungaji majina mabaya ulivyo fasheni ya kushughulikiana, yanayotokea sasa ni matunda ya mbegu iliyopandwa muda mrefu. Ikamwagiliwa maji, mche ukastawi. Sasa ni mavuno makubwa.
Ni ushuhuda jinsi karma inavyodai madeni yake. Inavyokuja ndivyo inavyoondoka, ikishabihiana na msemo “what comes around goes around”, kama alivyoandika Eddie Stone, katika kitabu chake kinachoitwa “Donald Writes No More”, ambacho ni chapisho la mwaka 1974.