Kompyuta yaipa Liverpool taji EPL

London, England. Ubashiri uliofanywa na kampuni ya Opta kupitia program ya kompyuta, umeipa Liverpool nafasi kubwa ya kutwaa ubingwa wa Ligi Kuu England (EPL) msimu huu kulinganisha na timu nyingine.

Kufanya vizuri kwa Liverpool katika mechi 11 ilizocheza kwenye EPL hadi sasa ikipata ushindi mara tisa na kutoka sare moja huku ikipoteza mechi moja, kumeifanya ijikusanyia asilimia nyingi za kipaumbele cha ubingwa katika ubashiri huo uliofanywa na Opta ikifuatiwa na Manchester City kisha Arsenal na timu nyingine.

Kwa mujibu wa Opta, ubashiri unaonyesha Liverpool ina asilimia 60.32 kwa sasa za kutwaa ubingwa wa Ligi Kuu ya England msimu huu, Manchester City ikiwa na asilimia 34.29 na Arsenal iko na asilimia 4.98 za kutwaa taji la EPL msimu huu.

Katika ubashiri huo, Chelsea imepewa asilimia 0.32 za kutwaa taji, Newcastle United ina asilimia 0.04, Brighton ina asilimia 0.01 wakati huo Tottenham Hotspur na Aston Villa kila moja ikipewa asilimia 0.02 ya kutwaa ubingwa.

Timu 12 hazijapewa asilimia yoyote ya kutwaa ubingwa wa EPL msimu huu ambazo ni Fulham, Man United, Nottingham Forest, Bournemouth, Brentford, West Ham United, Crystal Palace, Everton, Wolves, Leicester City, Ipswich na Southampton.

Utabiri huo haujaishia katika kubashiri asilimia za ubingwa tu bali pia hata idadi ya pointi ambazo kila timu inaweza kumaliza nazo mwishoni mwa msimu.

Liverpool imebashiriwa kumaliza ikiwa imekusanya idadi ya pointi 85.46, pointi 82.45 kwa Manchester City huku Arsenal ikitabiriwa kumaliza msimu ikiwa imekusanya idadi ya pointi 74.5 na Chelsea pointi 66.08.

Katika ubashiri wa kushuka daraja, kinara ni Southampton ambayo ina asilimia 94.90 ikifuatiwa na Ipswich yenye asilimia 70.70 za kushuka daraja na Leicester City ipo nafasi ya tatu kwa kuwa na asilimia nyingi za kushuka ikiwa na asilimia 46.83.

Kwa timu nne ambazo zitafuzu kucheza Ligi ya Mabingwa Ulaya msimu ujao, utabiri huo umeangukia kwa Liverpool, Manchester City, Arsenal na Chelsea.

Liverpool imeonekana kuanza vyema msimu huu ikiwa chini ya Slot ambapo inaongoza msimamo wa EPL ikiwa imekusanya pointi 28 huku Manchester City inayofuatia ikiwa na pointi 23.

Pia Liverpool inaongoza msimamo wa Ligi ya Mabingwa Ulaya ikiwa imekusanya pointi 12 katika mechi nne ambazo imecheza hadi sasa.

Timu hiyo haijapoteza mechi 13 mfululizo za mashindano tofauti ambapo imepata ushindi katika michezo 12 na kutoka sare mara moja.