
Ni msimu unaoonekana kuwa mbaya zaidi kwa mashabiki wa Manchester United kutokana na mwenendo usioridhisha wa timu hiyo.
Mashetani Wekundu wamejikuta wakianguka hadi katika nafasi ya 15 kwenye msimamo wa Ligi Kuu England (EPL) baada ya kupokea kichapo cha bao 1-0 kutoka kwa Tottenham Hotspur, juzi Jumapili.
Bao la mapema la Spurs la James Maddison ambalo lilifungwa kwenye mechi hiyo, limeifanya Manchester United ijikute katika nafasi ambayo iko jirani na nafasi tatu za chini ambazo timu zitakazomaliza hapo zitashuka daraja.
Hata hivyo wakati mashabiki wa Manchester United wakiwa na wasiwasi kutokana na uwezekano wa kushuka daraja, utabiri uliofanywa na kompyuta maalum ya kampuni ya takwimu ya Opta umeibakisha Man United katika EPL na kutoitabiria katika kundi la timu zitakazoshuka.
Kompyuta hiyo ya Opta imetabiri kuwa Manchester United ambayo kwa sasa iko katika nafasi ya 15 kwenye msimamo wa ligi ikiwa na pointi 29 baada ya mechi 25, itamaliza ligi msimu huu ikiwa katika nafasi ya 14 kwenye msimamo wa ligi hiyo.
Kwa mujibu wa utabiri huo, hakuna uwezekano wa Manchester United’s kumaliza ikiwa bingwa wala kuingia katika kundi la timu tano za juu kwenye msimamo wa EPL.
Timu hiyo imepata asilimia chache za kuingia katika nafasi 10 za juu ambapo kupitia utabiri wa kompyuta hio ina asilimia 5.5 tu za kufanya hivyo hadi sasa.
Utabiri huo umeipa Liverpool nafasi ya kwanza kuwa bingwa ikifuatiwa na Arsenal kisha Nottingham Forest na Manchester City.
Timu tatu ambazo zimetabiriwa zitashuka daraja ni Ipswich, Leicester City na Southampton.