Kombo awataka maofisa wa Polisi Zanzibar kujitafakari kukithiri uhalifu

Unguja. Kamishna wa Polisi Zanzibar, Kombo Khamis Kombo amewataka maofisa na wakaguzi wa Polisi kujitafakari kutokana na kuwepo kwa matukio ya uhalifu katika shehia wakati wao wapo huko.

Amesema hatua hiyo inaonyesha wazi wapo baadhi ya maofisa hao watimizi wajibu kwani kusingekuwa na matukio ya uhalifu kwa namna yanavyotokea.

Kombo ametoa kauli hiyo leo Februari 14, 2024 mjini Unguja kwa maofisa, wakaguzi na askari wa Jeshi la Polisi wa mikoa mitatu ya Unguja, ikiwa ni mara ya kwanza tangu ateuliwe katika nafasi hiyo, Desemba 2024.

“Haipendezi mkaguzi wa shehia, kwa kule bara wanaitwa polisi kata, kila siku inatajwa shehia yako katika matukio ya uhalifu, sasa kama wewe upo hapo unachukua hatua gani? Na unaonekana haikuumizi,” amesema Kombo.

Amewataka kuhakikisha wanashirikiana vema na jamii na kuwapa nafasi wananchi kushiriki katika kulinda amani kwenye maeneo yao kwani wanajua dhana nzima ya polisi jamii hasa vikundi shirikishi.

“Ulinzi bora unahakikisha unashirikiana na jamii, kwa hiyo tuwape nafasi wananchi kushiriki katika kulinda amani, tuwape nafasi katika ulinzi shirikishi ili wananchi watahisi wao ni sehemu ya suluhisho la changamoto zinazowakabili,” amesema.

Kwa mujibu wa taarifa ya Polisi iliyotolewa na Naibu Mkurugenzi wa Upelelezi wa Makosa ya Jinai, Zuberi Chembela, mwaka 2024 yalitokea matukio 1,116 katika vituo vya polisi, kati ya matukio hayo, ya mauaji yalikuwa 66.

Akizungumza kwa niaba ya makamanda wenzake, Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kaskazini Unguja, Benedict Mapujila amesema wataendelea kuhakikisha hali ya usalama inakuwapo na kufuatilia uadilifu kwa askari wanaowasimamia.

“Tutafuatilia maadili na suala la nidhamu kuhakikisha kwamba wanapaswa kutekeleza watu wote wanatekeleza na tutaongeza ushirikiano na vikundi vya ulinzi shirikishi na kusimamia changamoto za usalama kadri tunavyoweza katika nafasi zetu,” amesema Kamanda Mapujila.