
DROO ya hatua ya robo fainali ya Kombe la Shirikisho (FA) imechezeshwa huku timu mbili za Championship, Stand United na Mbeya City zikipangiwa kucheza dhidi ya wakongwe wa Ligi Kuu Bara, Yanga na Simba.
Katika droo hiyo iliyofanyika leo Alhamisi, Yanga itakuwa mwenyeji wa Stand United iliyopo nafasi ya tatu katika msimamo wa Championship baada ya kucheza mechi 25, huku wafungaji wenye mabao mengi kikosi kwao ni Omary Issa na Seleman Richard wote wana saba, tofauti na Yanga iliyopo kileleni mwa Ligi Kuu Bara kwa alama 58 ikicheza mechi 22, vinara wa mabao ni Clement Mzize na Prince Dube kila mmoja anayo 11.
Yanga ina wachezaji wazoefu wanaocheza timu za mataifa mbalimbali baadhi ni kipa Djigui Diarra (Mali), Stephane Aziz Ki (Burkina Faso), Clatous Chama, Kennedy Musonda (Zambia), Dickson Job, Ibrahim Bacca, Mzize, Bakari Mwamnyeto (Taifa Stars), hilo linawapa asilimia kubwa ya kuifanya Stand United kuingia uwanjani ikiwa ni timu ndogo ambayo haina wachezaji wa viwango kulinganisha na wapinzani wao ingawa katika soka lolote linaweza kutokea.
Kwa upande wa Simba, itakutana na Mbeya City iliyopo nafasi ya pili katika msimamo wa Championship, ikiwa imecheza mechi 25 huku wachezaji wanaoongoza kwa mabao ni Williams Thobias (tisa) na Eliud Ambokile ambaye ana uzoefu amepita timu kama TP Mazembe, Nkana, Leopards za Zambia akifunga mabao manane.
Simba iliyopo nafasi ya pili kwenye ligi, anayeongoza kwa mabao ni Jean Charles Ahoua aliyefunga 12 na Steven Mukwala anayo tisa huku kikosi chao kina wachezaji wengi wazoefu eneo la ulinzi kama Shomari Kapombe na Mohamed Hussein ‘Tshabalala’ wanaoweza kuwa mwiba wa kuwazuia washambuliaji wa Mbeya City.
Timu nyingine zinazocheza hatua hiyo ni JKT Tanzania dhidi ya Pamba Jiji ambazo zinashiriki Ligi Kuu Bara, zilipokutana mechi ya kwanza zilitoka suluhu na bado hazijarudiana mzunguko wa pili.
Pia Singida Black Stars itaikaribisha Kagera Sugar, mechi nyingine inayozikutanisha timu za ligi kuu.
Ili kupatikana timu zitakazocheza nusu fainali, mshindi kati ya Yanga na Stand United atakutana na mshindi kati ya JKT Tanzania na Pamba Jiji.
Nusu fainali nyingine itakuwa mshindi baina ya Simba na Mbeya City dhidi ya Singida Black Stars na Kagera Sugar.
Michezo ya robo fainali inatarajiwa kupigwa kati ya Aprili 10 hadi 14 mwaka huu.
Ofisa Habari wa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), Clifford Ndimbo, amesema: “Zimepangwa tarehe hizo, lakini itategemeana na ratiba za timu nyingine ambazo zitakuwa na michezo mingine.”
Kwa upande wa Mtendaji Mkuu wa JKT Tanzania, Jemedari Said Kazumari itakayocheza na Pamba, alisema: “Utakuwa mchezo mgumu kwani timu zote zinacheza Ligi Kuu na mechi ya kwanza ya ligi tulitoka suluhu, kabla ya kurudiana inatakiwa Pamba itufuate kwa ajili ya robo fainali ya FA, tunatarajia ushindani mkali na tunaamini tutafika mbali.”
Makamu Mwenyekiti wa Fedha wa Singida Black Stars, Omary Kaya alisema: “Tunatarajia ushindani, ninachokitamani ni kukutana na Simba nusu fainali, maana kuifunga timu kubwa kuna raha yake.”
Kocha mpya wa Mbeya City, Malale Hamsini alisema:
“Timu zikifika robo fainali hakuna wepesi, tulikuwa tunasubiri kujua wapinzani wetu, tumejua ni Simba tunajipanga kwa ajili ya Simba na siyo timu nyingine.”