Kombe la Muungano vita ya Bara, Visiwani

PAZIA la michuano ya Kombe la Muungano, linafunguliwa Alhamisi hii kwa mchezo mmoja wa robo fainali ambapo Singida Black Stars itaanza kampeni ya kusaka taji hilo dhidi ya JKU, saa 11:00 jioni.

Singida ni kati ya timu nane zinazoshiriki mashindano hayo msimu huu, huku ikipata nafasi hiyo baada ya kikosi cha Simba kujitoa kutokana na ratiba kubana ya Kombe la Shirikisho Afrika inayoshiriki ikiwa imefikia hatua ya nusu fainali.

Katika mchezo huo utakaopigwa kwenye Uwanja wa Gombani kisiwani Pemba, timu zote zinaingia zikiwa zinasaka rekodi mpya ya kuchukua ubingwa wa michuano hiyo kwa mara ya kwanza, kwani hazijawahi kufanya hivyo tangu ilipoanza kuchezwa mwaka 1982.

Akizungumzia mchezo huo, Kaimu Kocha Mkuu wa Singida Black Stars, David Ouma alisema kitendo cha kupata nafasi hiyo kimewapa nguvu ya kutumia mashindano hayo kama sehemu mojawapo ya kujiweka fiti na michezo mbalimbali iliyosalia pia ya Ligi Kuu.

“Hii ni nafasi nyingine kwetu ya kuonyesha ukubwa wa Singida, sisi hatuendi Zanzibar ili kushiriki bali tumekuja pia kwa lengo la kuchukua ubingwa huo, naamini kwa kikosi tulichonacho tunaweza kufanikisha azma yetu,” alisema Ouma.

Ofisa Habari na Mawasiliano wa Singida Black Stars, Hussein Massanza alisema wachezaji wote wako tayari kwa ajili ya mashindano hayo, japo watamkosa kinara wa ufungaji raia wa Ghana, Jonathan Sowah aliyefunga mabao 11 Ligi Kuu Bara.

“Mbali na Sowah wengine ni kiungo mshambuliaji, Marouf Tchakei na beki wa kushoto, Ibrahim Imoro kwa sababu za kiufundi zaidi, tumeenda na wachezaji tunaowaamini watatupigania ili kubeba kombe hili la Muungano,” alisema Massanza.

Mshindi wa mchezo huo atafuzu hatua ya nusu fainali ambapo atakutana na mshindi kati ya mabingwa wa michuano hiyo mwaka 1984, KMKM au Azam FC zitakazopambana Ijumaa saa 1:15 usiku kwenye Uwanja wa Gombani, Pemba.

Michuano hii inafanyika mwaka wa pili mfululizo kufuatia kufanyika pia 2024, baada ya kutofanyika kwa kipindi cha miaka 22, tangu mara ya mwisho ilipofanyika 2002, huku Yanga na Simba zikiongoza kuchukua taji hilo mara sita kila mmoja wao.

Bingwa mtetezi wa michuano hiyo ni Simba iliyochukua taji hilo mwaka jana, huku msimu huu ikishirikisha timu za Azam FC, Coastal Union, Singida na Yanga kwa Bara, ambapo kwa visiwani Zanzibar zinawakilishwa na JKU, KMKM, KVZ SC na Zimamoto.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *