
Shirikisho la Mpira wa Miguu Zanzibar (ZFF), limehamisha uwanja wa mashindano ya Kombe la Muungano na sasa yatachezwa katika Uwanja wa Gombani, Pemba.
Awali, shirikisho hilo lilitangaza kuwa mashindano ya Kombe la Muungano yataanza keshokutwa, Jumatano, Aprili 23, 2025 katika Uwanja wa New Amaan Complex mjini Unguja kabla ya kutoa taarifa ya kuyahamishia Pemba.
Uwanja huo ni miongoni mwa viwanja vinavyotarajiwa kutumiwa kwa ajili ya mashindano ya fainali za mashindano kwa timu za taifa kwa wachezaji wa ndani maarufu kama Chan.
Katika taarifa iliyotolewa leo Aprili 21, 2025 na Kaimu Ofisa Habari wa ZFF, Issa Chiwilem, imesema kuwa ZFF imepokea barua pepe (email) kutoka Shirikisho la Mpira wa Miguu Afrika (CAF) juu ya maelekezo ya kitaalamu ya matumizi ya uwanja huo.
“Uwanja wa New Amaan Complex kwa sasa umeingia katika mfumo maalumu wa matumizi, taarifa ya CAF imebainisha kuwa uwanja huo haushauriwi kuchezwa kwa mashindano yenye mechi nyingi mfululizo,” imesema taarifa hiyo.
Hivyo katika kutekeleza agizo hilo, taarifa hiyo imesema mashindano ya Muungano mwaka huu yatachezwa Gombani kisiwani Pemba.