
Dar es Salaam. Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG), Charles Kichere amesema makusanyo yote ya kodi yalichangia asilimia 56 ya mapato yote ya Serikali kwa mwaka wa fedha 2023/24.
Amesema ukaguzi wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) umebaini kwa mwaka huo wa fedha jumla ya makusanyo yalifikia Sh26.07 trilioni ikilinganishwa na Sh22.58 trilioni zilizokusanywa katika mwaka wa fedha 2022/23.
CAG ameyasema hayo leo Alhamisi, Machi 27, 2025 alipokuwa akisoma ripoti yake kuhusu mwenendo wa deni la Serikali wakati akikabidhi ripoti hiyo kwa Rais Samia Suluhu Hassan ya mwaka wa fedha 2023/2024 Ikulu jijini Dar es Salaam.
CAG amesema ukaguzi wa TRA umebaini kwa mwaka wa fedha 2023/2024 jumla ya makusanyo yalifikia Sh26.07 trilioni ikilinganishwa na Sh22.58 trilioni zilizokusanywa katika mwaka wa fedha 2022/23.
“Hili ni ongezeko la Sh3.49 trilioni ambalo ni sawa na ongezeko la asilimia 15.46 licha ya ongezeko hili makusanyo haya yalikuwa chini kwa Sh659.61 bilioni ambao ni sawa na sawa na asilimia 2.5 ya makadirio ya 26.725 trilioni makusanyo yote ya kodi ambayo yalichangia asilimia 56 ya mapato yote ya serikali,” amesema.
Aidha CAG amewapongeza TRA kwa juhudi zao za kukusanya mapato na kukaribia kufikia malengo ambayo yamekuwa yakiwekwa na Serikali.
Katika hatua nyingine, Kichere amesema Mamlaka ya Serikali za Mitaa zimekusanya Sh1.23 trilioni ambayo ni sawa na makisio ya Sh1.14 trilioni na kwamba halmashauri 110 zilivuka malengo yao ya makusanyo huku halmashauri 72 zikishindwa kufikia malengo.
“Nimebaini mapungufu kadhaa katika ukusanyaji wa mapato ikiwemo kesi zinazosubiri uamuzi za Sh9.85 trilioni, TRA ilikuwa na kesi za mapato 1,186 za kodi zenye jumla Sh9.83 trilioni zilizokuwa bado hazijatatuliwa na mahakama za mapato,” amesema.
Amesema katika Serikali za mitaa mamlaka 14 zilitarajiwa kukusanya Sh45.61 bilioni kupitia mawakala wa mapato lakini zilikusanya Sh19.49 bilioni ikiwa ni upungufu wa Sh26.12 bilioni.
CAG amesema amebaini upungufu mkubwa katika halmashauri ikiwemo Halmashauri ya Jiji la Dar es Salaam ambayo ilipaswa kukusanya kutoka kwa mawakala kiasi cha Sh15 bilioni lakini ilikusanya Sh3.4 bilioni.
Halmashauri ya Kinondoni ilipaswa kukusanya Sh10.25 bilioni lakini ilikusanya Sh5 bilioni. Ubungo Sh3.1 bilioni ilikusanya Sh909 mililioni. Mwanza Sh3.6 bilioni ikafanikia kukusanya Sh1.6 bilioni, Kibondo Sh2.1 bilioni ikakusanya Sh635 milioni na Babati Sh2.5 bilioni ilikusanya Sh1.47 bilioni.
“Napendekeza menejimenti za mamlaka husika zisimamie kwa karibu utekelezaji wa mikataba na kuhakikisha zinajumuisha vipengere vya fidia kwa dhamana, ili kusaidia pale mawakala wanaposhindwa kutimiza masharti ya mikataba,” amependekeza CAG.