
KUNA rekodi mbili ziko ndani ya uwezo wa Kocha wa Yanga, Miloud Hamdi lakini zina mtego.
Kocha huyo raia wa Algeria anaweza kuvunja rekodi ya pointi na mabao ya timu hiyo kwa msimu uliopita wa Ligi Kuu Bara. Itawezekanaje? Anatakiwa kuvuna pointi kwenye kila mchezo uliopo mbele yake.
Msimu uliopita, Miguel Gamondi aliiwezesha Yanga kumaliza na pointi 80, huku wakifumania nyavu mara 71. Lakini chini ya Hamdi, Wananchi wanaonekana kuwa na moto mkali tangu arithi mikoba Sead Ramović.
Kufikia raundi ya 22, Yanga SC tayari ina pointi 58 na mabao 58, ikiwa na mechi nane mkononi. Hili linaashiria kuwa wanayo nafasi kubwa ya kuzidi rekodi za msimu uliopita, endapo wataendelea na kasi waliyonayo.
Tangu atue Yanga, Hamdi ameiongoza timu hiyo katika michezo mitano ya ligi, akishinda minne na kutoa sare moja. Timu yake imefunga mabao 16 na kuruhusu mabao mawili tu, ikiwa na rekodi ya ushindi kwa asilimia 80. Hii ni ishara kuwa ana uwezo mkubwa wa kubadili upepo wa Yanga na kuifanya kuwa timu tishio zaidi.
Katika mechi zilizosalia, Yanga inakutana na Tabora United, Coastal Union, Azam FC, Fountain Gate, Namungo, Tanzania Prisons, na Dodoma Jiji. Ukiongeza na mechi ya kiporo dhidi ya Simba SC, ni wazi kwamba Yanga ina nafasi ya kuendelea kuvuna pointi nyingi zaidi na kuongeza idadi ya mabao.
Hamdi tayari ameonyesha uwezo wake wa kushambulia kwa kasi na kubadilika kulingana na wapinzani wake. Kwenye mzunguko wa kwanza, Yanga ilipoteza pointi dhidi ya Tabora United kwa ushindi wa 3-1 na dhidi ya Azam FC kwa kipigo cha 1-0. Ikiwa watahakikisha wanavunja mwiko huo na kupata ushindi katika mechi hizi za marudiano, basi rekodi mpya zinaweza kuwekwa.
Kwa wastani wa sasa wa mabao 2.63 kwa mchezo, endapo Yanga itaendelea na kasi hii, wanayo nafasi nzuri ya kuvuka mabao 71 ya msimu uliopita. Ikiwa timu hiyo itafanikiwa kufunga angalau mabao 14 kwenye mechi zilizobaki, basi wataandika historia mpya kama timu iliyofunga mabao mengi zaidi ukilinganisha na msimu uliopita katika wa Ligi Kuu Tanzania Bara.
Kwa upande wa pointi, Yanga inahitaji angalau pointi 23 kati ya 24 zinazowezekana ili kuvuka rekodi ya msimu uliopita. Ikiwa wataendelea na ushindi mfululizo, basi kuvuka alama 80 kutakuwa jambo la uhakika, na huenda wakamaliza ligi wakiwa na zaidi ya pointi 81.
Lakini changamoto ipo, hasa kwenye mechi dhidi ya Azam FC na Simba SC. Azam, ambayo tayari iliwapiga Yanga kwenye mzunguko wa kwanza, haitakuwa kazi rahisi, huku Simba ikiwa tishio hasa kwa vile mechi yao bado haijapangiwa rasmi kutokana na mvutano uliopo.
Hata hivyo, Hamdi anaweza kutumia uzoefu wake wa kimataifa kuhakikisha Yanga inavuka vizingiti hivi bila madhara.
Nguvu ya Hamdi inatokana na mbinu zake za kushambulia kwa kasi, nidhamu ya kiufundi, na uwezo wake wa kufanya mabadiliko ya haraka kulingana na mahitaji ya mchezo. Chini yake, Yanga imekuwa na mwitikio mzuri, huku washambuliaji wake wakionyesha ubora wa hali ya juu.
Mafanikio ya kuvunja rekodi hizi mbili hayatatokana na Hamdi pekee, bali pia mshikamano wa kikosi chake. Wachezaji kama Stephane Aziz Ki, Pacome Zouzoua, Prince Dube na Clement Mzize wamekuwa nguzo muhimu katika mafanikio ya timu. Hawa ndio watakaobeba majukumu makubwa kuhakikisha Yanga inafanikisha malengo yake.
Hata hivyo, kocha Hamdi anaamini kuwa mafanikio haya hayawezi kufikiwa bila umoja wa kweli wa timu.
“Tunajivunia kile ambacho tumekifanikisha hadi sasa, lakini bado kuna kazi kubwa mbele yetu. Huu ni msimu muhimu, na tunahitaji kuwa na umakini wa hali ya juu ili kufikia malengo yetu. Rekodi mbili muhimu ziko kwenye uwezo wetu, na kwa bidii, nidhamu, na kushirikiana kama timu, naamini tunaweza kuzivunja,” alisema Hamdi.
Kocha huyo aliongeza kwa kusema; “Yanga ni timu kubwa, na hatujafika hapa kwa bahati. Kila mchezo ni changamoto, lakini kila mchezaji anajua majukumu yake. Huu ni wakati wa kuonyesha umwamba wetu na kuandika historia. Tumekubaliana kwamba hatutakubali kushindwa. Tutapambana kwa kila kitu tunachokimiliki.”
Miloud Hamdi pia anaonyesha ujasiri wake kwa kutoa nafasi kwa wachezaji wake. “Hii ni kazi ya pamoja. Kila mmoja anafanya kazi yake kwa bidii. Tutaendelea kushikamana na kufanikisha malengo.”