
YANGA inacheza na Songea United Jumamosi hii saa 10 jioni kwenye mechi ya FA. Lakini Kocha Hamdi Miloud kuna kitu amekiona kwa winga Mkongomani aliyesajiliwa dirisha dogo, Jonathan Ikangalombo akalazimika kutamka kitu na kuwaambia mashabiki wavute pumzi.
Staa huyo alitupia kwenye mechi ya kirafiki dhidi ya Singida Black Stars hivi karibuni na kuibuka mjadala miongoni mwa mashabiki wakivutia na staili yake ya uchezaji.
Kocha huyo ameliambia Mwanaspoti kuwa bao ambalo Ikanga Speed aliwafunga Singida Black Stars ni kama mwanzo tu wa mambo matamu ambayo ameanza kuyaonyesha kwani kuna mazuri yatakuja.
Miloud alisema kuwa hana shaka na ubora wa Ikangalombo kwani Mkongomani huyo, amethibitisha kipaji chake mara tu alipokuwa anamuona uwanjani akijiridhisha kwamba jamaa ni fundi.
Kocha huyo alisema kuwa kadri anavyoendelea kuimarika Ikangalombo ataonyesha mambo makubwa ambayo wao wameshaanza kuyaona wakiwa mazoezini.
“Labda wengine huko nje ndio wana wasiwasi na Ikangalombo, lakini kwetu sisi tulio ndani tunajua na tulishajiridhisha kwamba, ana kipaji kikubwa sana,” alisema Miloud ambaye ni kocha mzoefu Afrika.
“Lile bao ambalo aliwafunga Singida ni kama sehemu tu ya mambo bora ambayo anayo lakini huu muda ambao tunaendelea kumpa atawatuliza wote ambao bado hawajagundua ukubwa wa kipaji chake.”
Aidha, Miloud alisema kwasasa anataka kuendelea kumuongezea muda winga huyo wa zamani wa AS Vita akisema ndani ya mechi chache zijazo atazidi kuongeza ushindani kwenye kikosi chake.
“Tutakuwa tunamuongezea muda taratibu, nadhani unaona akiingia uwanjani anaonyesha njaa ya kutaka kufanya mambo makubwa, nataka mchezaji mwenye akili kubwa kama hii, juhudi anazofanya zitaifanya timu kuongeza ushindani wa nafasi.”