Kocha wa Stars aibukia Rwanda

WAKATI Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), likisubiri kujua hatma ya kocha mkuu wa timu ya Taifa Stars, Adel Amrouche, mwenyewe ameshtua kwa kuibukia Rwanda.

Shirikisho la Soka Rwanda (Ferwafa), limemtangaza mchana huu Amrouche, kuwa kocha wa timu ya Taifa hilo maarufu kama ‘Amavubi’.

Mbali na Amrouche, Ferwafa imewatangaza makocha wawili wazawa, Erick Nshimiyimana atakayekuwa msaidizi wa kwanza wakati Dk Carolin Braun akiwa msaidizi wa pili.

Taarifa hiyo pia, imemtangaza kocha Casa Mbungo, kuwa kocha wa timu ya wanawake ambaye pia atakuwa akisimamia maendeleo ya soka chini ya kurugenzi ya ufundi.

Hatua hiyo ya Amrouche, inakuja zikiwa zimepita wiki chache tangu kocha huyo ashinde kesi yake dhidi ya Shirikisho la Soka Afrika (CAF), hukumu iliyotakiwa kumlipa fidia kocha huyo.

Sintofahamu ya Amrouche kujiunga na Amavubi, inakuja kufuatia kocha huyo kuwa ndani ya mkataba na TFF, ambao unamalizika mwakani.

Kufuatia taarifa hiyo, viongozi wa TFF hawakupatikana kuizungumzia sintofahamu hiyo.

Amrouche alikumbana na adhabu ya kusimamishwa mechi nane baada ya kukutwa na hatia ya kutoa kauli ya kichochezi dhidi ya Shirikisho la Soka la Morocco siku chache baada ya Tanzania kufungwa 3-0 na Morocco katika mechi ya kwanza ya fainali za Kombe la Mataifa ya Afrika (Afcon) 2023 zilizofanyikia Ivory Coast.

Kocha huyo alinukuliwa na televisheni ya Algeria anakotokea, akisema; “Shirikisho la Morocco ni nguvu iliyothibitishwa katika ulimwengu wa soka ya Afrika. Morocco inasimamia soka ya Afrika,” Amrouche aliiambia runinga moja nchini Algeria katika mahojiano kabla ya Kombe la Mataifa 2023 kuanza nchini Ivory Coast.

Amrouche mzaliwa wa Algeria alidai maafisa wa Morocco ndani ya CAF huamua ni nani waamuzi wa mechi zinazohusisha timu ya taifa ya wanaume ya Morocco, na muda wa mechi kuanza, ndipo akaadhibiwa kwa kutoa faini ya Dola 10,000 na kusimamishwa mechi nane na TFF nayo ikatangaza kumsimamisha na timu kuachwa chini ya makocha wazawa, Hemed Morocco na Juma Mgunda.