
London, England. Baada ya kudumu kwa miaka 18 kwenye kikosi cha Chelsea kocha wa makipa wa timu hiyo, Hilario ameachia ngazi.
Kocha huyo mwenye uwezo wa juu, ameachana na timu hiyo ili aweze kujiunga na Thomas Tuchel kwenye kikosi cha timu ya Taifa ya England.
Tuchel ataanza kazi yake kama kocha mkuu wa taifa hilo kubwa duniani Januari 1, 2025 na ameanza kutengeneza benchi bora la kuungana naye akiwamo Hilario.
Kipa huyo wa zamani wa alitumikia kwenye kikosi cha Chelsea kwa michezo 39 kuanzia mwaka 2006 hadi 2014.
Ataungana kwenye kikosi cha England na makocha wengine wa zamani wa Chelsea, Anthony Barry na James Melbourne.
Chanzo kutoka Chelsea kimesema kuwa kocha huyo ameondoka na sasa timu hiyo ipo kwenye mchakato wa kujaza nafasi yake huku Michele De Bernardin akiwasili kutoka Leicester kusaidiana na Enzo Maresca kwenye timu hiyo ambayo imekuwa ikionyesha kiwango cha juu uwanjani.
Tuchel amepewa mkataba wa miezi 18 kwenye timu hiyo akiwa anachukua nafasi ya Gareth Southgate ambaye alifanya makubwa na kikosi hicho.
Moja ya malengo ambayo Tuchel amepewa ni kuhakikisha anaipa timu hiyo ubingwa wa Kombe la Dunia 2026, kazi ambayo alipewa Southgate ikamshinda.