Kocha Stellenbosch awahofia Mpanzu, Kibu

KOCHA wa Stellenbosch FC, Steve Barker, ameanza kuingiwa ubaridi kabla ya kuvaana na Simba katika mechi ya nusu fainali ya Kombe la Shirikisho Afrika, akiwataja Kibu Denis na Elie Mpanzu kuwa ndio wanamtia tumbo.

Mchezo wa kwanza wa nusu fainali hiyo utafanyika Aprili 20 jijini Dar es Salaam, ambapo Simba imekuwa ikitumia vizuri uwanja huo kama ngome isiyotikisika. 

Takwimu zinaonyesha kuwa Simba imekuwa ikifunga wastani wa mabao mawili au zaidi kwenye kila mchezo wa kimataifa walioucheza hapo msimu huu tangu hatua ya awali ya mashindano haya.

Akizungumza ikiwa ni siku chache tangu awang’oe mabingwa mara tano wa Ligi ya Mabingwa Afrika, Zamalek, Barker alikiri kuwa na kibarua kizito kwa  kazi iliyoko mbele yao, hasa kwa namna Simba ilivyo na rekodi nzuri nyumbani na kiwango cha wachezaji wao tegemeo.

“Simba ni timu yenye uzoefu mkubwa wa michuano ya Afrika na wana wachezaji hatari ambao wakipata nafasi, wanakuadhibu. Mpanzu ni mshambuliaji wa kiwango cha juu, pamoja na Kibu. Ana kasi, anacheza kwa nguvu hilo tunalitambua,” alisema Barker.

Kibu Denis, ambaye ni miongoni mwa nyota wanaong’ara kwenye kikosi cha Simba msimu huu, ana mabao matatu kwenye Kombe la Shirikisho Afrika, ikiwa ni mabao mawili pungufu tu ya kinara wa mabao kwenye michuano hiyo, Ismail Belkacemi wa USM Alger (5 mabao). Belkacemi ameshatolewa baada ya timu yake kufungwa na CS Constantine, jambo linaloweka nafasi kubwa kwa Kibu kuendelea kusogea juu kwenye mbio za Kiatu cha Dhahabu.

Kwa upande mwingine, Barker amekiri kuwa mchezo wa kwanza ugenini unaweza kuwa na presha kubwa kwa wachezaji wake, hasa mbele ya mashabiki wa Simba ambao wamekuwa silaha ya ziada kwa timu yao kila wanapocheza nyumbani.

“Hatupaswi kuingia uwanjani kwa kujiamini kupita kiasi. Tunapaswa kuwa makini, kupunguza makosa na kuamini katika mipango yetu ya kiufundi. Tunajua Benjamini Mkapa ni moto lakini nusu fainali inahitaji roho ya chuma,”  alisema kocha huyo.

Mchezo wa marudiano utapigwa Aprili 27 nchini Afrika Kusini, lakini tayari Barker amesisitiza kuwa matokeo ya mechi ya kwanza yatakuwa na nafasi kubwa ya kuamua hatima ya timu yake.

Kwa sasa, Stellenbosch wanajiandaa kwa mtihani mgumu mbele ya Simba ambayo imeonyesha ukomavu mkubwa katika hatua za mtoano, ikiifunga Al Masry ya Misri kwa mikwaju ya penalti 4-1 baada ya kusawazisha mabao 2-0 ambayo waliruhusu kwenye mchezo wa robo fainali ya kwanza, Misri.

Je, Simba wataendeleza ubabe wao kwenye Benjamini Mkapa, au Stellenbosch ya Barker itaweza kusimama imara na kuzuia moto wa Wekundu wa Msimbazi? Macho yote yatakuwa Dar es Salaam Aprili 20.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *