Kocha Simba Queens atoa neno

KOCHA Mkuu wa kikosi cha Simba Queens, Yussif Basigi amesema timu hiyo inapaswa kuwa makini na michezo iliyosalia ya Ligi Kuu ya Wanawake.

Wikiendi iliyopita timu hiyo ilipoteza ikiwa nyumbani dhidi ya mtani wake Yanga Princess kwa bao 1-0 uwanjani KMC Complex ikiwa ni mechi ya kwanza kwa kocha huyo Mghana kupoteza tangu kutua nchini msimu huu.

Basigi ambaye alichukua mikoba ya Juma Mgunda aliyetimuliwa kikosini hapo Agosti mwaka jana, kwenye michezo 13 aliyosimama kama kocha mkuu, ameshinda 11 sare moja na kupoteza moja.

Akizungumza na Mwanaspoti, Basigi alisema kama timu wanapaswa kuwa makini kwenye michezo mitano iliyosalia kuhakikisha wanapata pointi zote na kuutetea ubingwa wao.

“Ligi ngumu ukipoteza tu pointi mshindani wako anasogea nafasi yako, tunapaswa kuweka umakini kwenye mechi tano zilizosalia na kuachana na matokeo ya nyuma,” alisema Basigi.  Simba imeshuka hadi nafasi ya pili ikitoka kileleni ambako sasa iko JKT Queens ikiwa na pointi 35 kwa tofauti ya alama moja na mnyama aliye na pointi 34 kisha Yanga Princess 27 kwenye michezo 13.

Mechi tano zimebaki kumaliza msimu.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *