Kocha Simba aipa ushindi Yanga akilitaja deni

SIKU zinavyosogelea Dabi ya Kariakoo inayotarajiwa kupigwa Machi 8, mwaka huu, ndivyo mambo yanavyozidi kuwa moto zaidi, huku mijadala juu ya kipute hicho cha raundi ya pili ya Ligi Kuu Bara ikishika kasi katika vilinge na vijiwe mbalimbali nchini.

Wakati mambo yakizidi kuwa mambo, wachezaji na makocha wakikuna vichwa, lakini kuna stori kibao zingine za kitaalamu zikiibuka kutoka kwa watu mbalimbali wakiutazama mchezo huo kwa jicho la tatu na matarajio yao yakijikita kwenye ufundi.

Kauli aliyoitoa kocha wa zamani wa Simba, Roberto Oliviera ‘Robertinho’ kwa Mwanaspoti katika mahojiano maalumu inaashiria kwamba Yanga ina nafasi kubwa ya kupata ushindi katika mchezo huo.

Kocha huyo ambaye alitumuliwa Simba Novemba 9, 2023 ikiwa ni siku chache baada ya kufungwa 5-1 na Yanga, alisema Wekundu hao wa Msimbazi kazi waliyonayo ni kubwa kuliko wapinzani wao hivyo wakizembea wanapokea tena kichapo.

Robertinho ambaye aliifundisha Simba kuanzia Januari 3, 2023, hadi anaondoka Novemba 9, 2023, ameacha rekodi ya kuwa kocha wa mwisho wa timu hiyo kupata ushindi dhidi ya Yanga na aliiongoza katika Kariakoo Dabi tatu akishinda mbili kwa maana ya Ligi Kuu na Ngao ya Jamii na kupoteza moja wa Ligi Kuu

Tangu alipoondoka kwa Robertinho, Simba haijaifunga Yanga katika kukutana kwao mara tatu (mbili ligi kuu na moja Ngao ya Jamii), chini ya makocha wawili, Abdelhak Benchikha na Fadlu Davids aliyepo sasa.

Akizungumza na Mwanaspoti, Robertinho amesema kwa vyovyote vile Simba ndiyo timu itakayoingia na deni kubwa mbele ya Yanga kwani imepita muda mrefu bila ya kuifunga, hivyo inapaswa kusahihisha makosa yao.

“Jumamosi hii kwa kuwa Simba haijaifunga Yanga tangu nilipowafunga mimi, ni wazi ni muda mrefu, hivyo lazima ipambane kupata ushindi,” amesema kocha huyo.

“Simba hawatakiwi kuingia kizembe, wacheze kwa malengo, wakikosea tu wanaweza kupoteza tena. Hata kipindi kile walipotufunga mabao matano hatukutaka, lakini ilitokea kutokana na makosa tuliyoyafanya kwa kuwaachia nafasi kubwa Yanga kutushambulia kwa nguvu.

“Yanga bado wana timu imara sana kuzidi Simba ingawa imeendelea kubadilika, lakini ni wazi kazi haitakuwa rahisi katika mchezo huo.”

KISA CHA KUONDOKA
Kocha huyo amezungumzia pia dabi ya Kariakoo akisema: “Sitasahau dabi ndiyo iliyoniondosha Simba na hiyo yote ni kwa sababu ya presha kubwa inayokuwepo kabla na baada ya mechi.

“Ifike mahala klabu zitambue kumwondosha kocha ni sawa na kuivuruga timu na mechi moja haiharibu ubora wa mwalimu.”

MECHI YA MTEGO
Yanga inakwenda kuikaribisha Simba katika mchezo huo wa Ligi Kuu Bara utakaochezwa Uwanja wa Benjamin Mkapa ukiwa ni wa mtego kwani yeyote atakayepoteza anaweza kujiweka hatarini katika kuwania ubingwa.

Hivi sasa Yanga ambao ni mabingwa watetezi wa ligi hiyo, wanaongoza msimamo wakiwa na pointi 58 baada ya michezo 22, inafuatiwa na Simba yenye pointi 54 ikicheza mechi 21. Bado mechi nane kwa Yanga kumaliza msimu huu wakati Simba ikibakiwa na mechi tisa.