Kocha Newcastle aweka rekodi England

London, England. Baada ya kuifunga Liverpool mabao 2-1 katika fainali ya Kombe la Carabao, Newcastle United imefanikiwa kutwaa taji hilo kwa mara ya kwanza tangu mara ya mwisho ilipobeba taji la Inter-Cities Fairs Cup mwaka 1969.

Katika mchezo huo uliochezwa kwenye Uwanja wa Wembley, Newcastle ilionyesha nia ya dhati ya kutwaa taji hilo, ambapo beki, Dan Burn alifungua ukurasa wa mabao kwa kuunganisha kichwa akimalizia mpira wa kona uliopigwa krosi na Kieran Trippier dakika ya 45.

Mshambuliaji Alexander Isak, aliongeza bao la pili dakika chache baada ya kipindi cha pili kuanza, akiunganisha pasi ya Bruno Guimarães.

Liverpool walijaribu kurejea mchezoni ambapo walipata bao la kufutia machozi kupitia kwa Federico Chiesa katika dakika za nyongeza, lakini juhudi zao hazikutosha kuzuia ushindi wa Newcastle.

Ushindi huu unakuwa wa kwanza kwa Newcastle tangu walipotwaa Kombe la Maonyesho la Miji mwaka 1969 na hivyo kurejesha furaha kwa mashabiki wao waliovumilia kwa muda mrefu.

Mashabiki wa Newcastle walifurika nje ya Wembley kushuhudia tukio hilo la kihistoria, wengi wao wakiwa hawana tiketi lakini walijaa kuunga mkono timu yao.

Kocha Eddie Howe amekuwa wa kwanza kutokea England kushinda taji la Carabao tangu Steve McClaren alipofanya hivyo akiwa na Middlesbrough mwaka 2004.

Baada ya kufunga bao kwenye fainali Dan Burn, amekuwa mchezaji wa tatu mwenye umri mkubwa kufunga bao katika mchezo wa fainali akiwa na miaka 33 na siku 311 tangu alipofanya hivyo Stoke George (35) wa Eastham mwaka 1972 pamoja na John Terry (34) wa Chelsea mwaka 2015.

Katika mchezo huo ilishuhudiwa nyota wa Liverpool Mohamed Salah kwa mara ya kwanza akiondoka dakika 90 bila kupiga shuti langoni wala kutengeneza nafasi yoyote.

Vinara wa kutwaa Carabao

Liverpool –          10

Manchester City- 8

Man United-      6

Chelsea –           5

Aston Villa-      5

Spurs –            4

Nottigham-     4

Leicester –       3

Arsenal-         3

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *