Kocha Matano ashtukia jambo Bara

KOCHA Mkuu wa Fountain Gate, Robert Matano amesema ana mtihani mkubwa wa kufanya kuikabili Simba kwenye mchezo wake wa kwanza akidai ni kipimo sahihi kwake.

Fountain Gate itakuwa wenyeji kwenye mchezo huo unaotarajiwa kuchezwa Februari 6, mwaka huu ukiwa ni mchezo 17 baada ya kucheza 16 wakikusanya pointi 20 na kushika nafasi ya sita.

Akizungumza na Mwanaspoti, Matano alisema anafurahishwa na mwendelezo mzuri wa wachezaji kuanza kuzoea mbinu zake baada ya kuingia kambini kwa ajili ya kujiandaa na mzunguko wa pili.

“Niliomba timu iingie mapema kutokana na mimi mwenyewe kutaka kukaa na timu ili niweze kutambua ubora wa mchezaji mmoja mmoja na pia kuwajenga kwenye mfumo ambao nimekuwa nikiutumia. Nafurahishwa na maendeleo ya wachezaji wangu,” alisema.

“Tukiwa kambini tulifanikiwa kupata mchezo mmoja wa kirafiki, tulicheza na Mbuni na kufanikiwa kuambulia ushindi wa mabao 2-1 sio mwanzo mbaya kwa sababu kuna makosa mengi yamepungua.”

Akizungumzia mchezo dhidi ya Simba, alisema hawatarajii urahisi lakini watapambana kuhakikisha wanatumia vyema uwanja wa nyumbani kukusanya pointi tatu.

“Tunakutana na timu kubwa ambayo ndio kinara wa msimamo. Hatutarajii mteremko tunajiandaa kuhakikisha hatufanyi makosa. Tunatarajia dakika 90 bora tumejiandaa kushindana na lengo ni kuhakikisha tunakusanya pointi tatu,” alisema.

Matano aliyeteuliwa kuiongoza timu hiyo Januari 10, mwaka huu akichukua nafasi ya Mohamed Muya, mwezi Februari anatarajia kuiongoza kwenye mechi sita sita.