
LIGI inatarajia kurejea keshokutwa ambapo kocha wa JKT Tanzania, Ahmed Ally ametaja mbinu tatu zitakazombeba kwenye mechi saba zilizobaki huku akitambia rekodi ya uwanja wa nyumbani kuwa hana shaka kwenye michezo mitano kati ya saba iliyobaki.
JKT Tanzania ipo nafasi ya sita kwenye msimamo baada ya kucheza mechi 23 ikikusanya pointi 30, ndio timu ambayo ilikuwa inashikilia rekodi bora ya timu ambazo hazijapoteza zikiwa nyumbani kabla ya Jonathan Sowah wa Singida Black Stars kuitibua Februari 13.
Kabla timu hiyo ilikuwa imecheza michezo tisa ya mashindano yote ambapo kati yake minane ni ya Ligi Kuu Bara na mmoja wa FA.
Akizungumza na Mwanaspoti, Ahmed alisema amezungumza na wachezaji wake kuendeleza rekodi ya kutokubali kuruhusu wapinzani kuuzoea uwanja wao wa nyumbani kwa kuhakikisha wanakuwa na staili ya kuwakaba kuanzia kwenye eneo lao la juu na kuwa na nidhamu ya hali ya juu ili kuweza kumaliza mechi tano kwa kishindo katika uwanja huo wa nyumbani.
“Nidhamu ni miongoni mwa vitu vya msingi vya kufanya ufikie malengo na matarajio. Nilitaka kuongoza mazoezi. Ilikuwa ni muhimu kuwaona wachezaji ukizingatia tunaelekea mwisho wa msimu tunahitaji kuwa kwenye nafasi nzuri zaidi bila kutazama nakutana na wapinzania wa aina gani,” alisema na kuongeza:
“Usahihi wa kutumia nafasi pia ni kitu muhimu sana kwetu hatuna wastani mzuri wa kufunga mabao lakini pia najivunia wachezaji wangu hasa wa eneo la ulinzi hawana makosa mengi hivyo napambana kuboresha zaidi eneo la ushambuliaji lakini pia kuzuia mashambulizi ya mara kwa mara langoni kwetu.”
Ahmed alisema anategemea kuona kila mchezaji wa JKT Tanzania anaipigania jezi ya klabu hiyo na kuwa mfano bora nje na ndani ya uwanja kwani ndio siri ya mafanikio ya klabu.
“Wachezaji niliokuwa nao mazoezini wanatakiwa kunionyesha kile walichonacho na wanachoweza kukifanya hivyo ni vizuri. Ni fursa muhimu kutazama ubora wao, lakini ni nafasi kwao kuonyesha kwamba wanastahili kuichezea JKT.
Kocha huyo aliongeza kuwa: “Ligi ni ngumu kila timu inahitaji matokeo kujihakikishia nafasi ya kucheza msimu ujao kwangu nazingatia zaidi ubora na nidhamu ili kuweza kumuadhibu mpinzani naamini hata wachezaji wangu wanafahamu nini tunakitaka.”