
KITENDO cha Coastal Union kutupwa nje ya mashindano ya Kombe la Muungano baada ya kuchapwa bao 1-0 dhidi ya Zimamoto katika hatua ya robo fainali, kaimu kocha mkuu wa kikosi hicho, Joseph Lazaro amesema nguvu zao wanazielekeza Ligi Kuu Bara.
Coastal Union ilikuwa timu ya pili kutoka Bara kuondoshwa katika mashindano hayo, baada ya awali Singida Black Stars iliyofungua pazia kutupwa nje kwa kuchapwa kwa mikwaju ya penalti 6-5 na JKU, kufuatia sare ya mabao 2-2.
Akizungumza na Mwanaspoti, Lazaro alisema sababu ya kuondoshwa mapema katika michuano hiyo ni kutokana na kutowajua vyema wapinzani wao, ingawa kwa sasa wanarudi kujipanga upya kwa michezo ijayo ya kumalizia msimu huu wa Ligi Kuu Bara.
“Hayakuwa malengo yetu kutolewa mapema namna hii, ingawa nawashauri waandaaji wabadilishe huu mfumo ili watoe nafasi ya timu zote kucheza zaidi ya mechi moja hadi kufikia mtoano, tumepoteza ila tunajipanga tena na Ligi Kuu,” alisema Lazaro.
Kocha huyo anayekaimu nafasi hiyo baada ya kuondoka kwa Juma Mwambusi, alisema hawatokuwa na mapumziko kwa wachezaji wa timu hiyo, kwani wanahitaji kumaliza vizuri mechi zilizobaki ili kuepuka kucheza mechi za mtoano kupambania kubaki kwenye ligi.
Lazaro ambaye awali alikuwa ni kocha msaidizi, alianza rasmi kukiongoza kikosi hicho Aprili 6, 2025, hadi sasa amekiongoza katika michezo minne na kati ya hiyo mitatu ni ya Ligi Kuu Bara na mmoja wa Kombe la Muungano.
Katika michezo mitatu ya Ligi Kuu Bara, Lazaro ameshinda miwili akizifunga Singida Black Stars na KenGold kila mmoja wao mabao 2-1, huku mmoja pekee ambao ulikuwa ndio wa kwanza kwake kikosini akipoteza kwa bao 1-0, dhidi ya Yanga, Aprili 7.
Mwingine mmoja ni wa Kombe la Muungano ambao amepoteza bao 1-0 dhidi ya Zimamoto, ambapo kwa sasa timu hiyo inajiandaa na mchezo ujao ugenini wa Ligi Kuu Bara mbele ya Tanzania Prisons, utakaopigwa Mei 12 kwenye Uwanja wa Sokoine jijini Mbeya.