Kocha Ali aahidi furaha Mashujaa Queens

KOCHA wa Mashujaa Queens, Ali Ali amesema amepambana kuhakikisha wachezaji wake wanakuwa sawa kisaikolojia baada ya vichapo viwili mfululizo kuwatoa mchezoni.

Mashujaa ilipoteza mechi mbili mfululizo dhidi ya Ceasiaa ugenini ikichapwa mabao 2-0 na Yanga Princess ikipoteza kwa mabao 2-1 nyumbani.

Matokeo hayo yaliifanya Mashujaa kusalia nafasi ya nne ikiwa na pointi 18, ikishinda mechi tano, sare tatu na kupoteza mechi nne dhidi ya JKT Queens na Simba Queens.

Ali Ali alisema mechi hizo ziliwatoa mchezoni wachezaji wake na aliporudi kwenye kiwanja cha mazoezi alipambana kurudisha hali ya kujiamini wakielekea kwenye mechi ngumu na JKT.

Aliongeza wanakutana na JKT moja ya timu alizowahi kuzifundisha hapo awali kwa mafanikio makubwa akikiri ugumu atakaokutana nao.

“Nimejaribu kupambana kuwarudisha mchezoni wachezaji wangu, mojawapo mwa malengo yetu ni kuhakikisha tunamaliza nafasi ya nne ingawa kuna ugumu kutokana na ligi kila mmoja akiitolea macho nafasi hiyo,” alisema Ali.

“Kila mmoja anafahamu ubora wa JKT ni mchezo mzuri na mgumu kwa upande wetu kutokana na ubora wa wachezaji, benchi la ufundi lakini tutapambana kwa uwezo wetu kuhakikisha tunaondoka na ushindi.”