
SIMBA inaendelea na hesabu zake ikijiandaa na mchezo wa Robo Fainali ya Kombe la Shirikisho Afrika, lakini kocha wa wapinzani Anis Boujelbene, ameliambia Mwanaspoti kikosi chake kipo kwenye mtego mkubwa.
Simba itakutana na Al Masry ya Misri, kwenye mchezo wa robo fainali ikianzia ugenini utakaopigwa Aprili 2, Jijini Suez sio mbali sana na Jiji la Cairo, kisha timu hizo zitarudiana hapa nchini Aprili 9,2025.
Wekundu hao ambao hatua ya makundi walikiwasha, huku wakiweka rekodi ya kufunga mabao nane na kuruhusu manne tu, wamewashtua waarabu hao ambao watacheza nao mchezo unaofuata.
Katika mabao hayo Simba imefunga matano katika uwanja wake wa nyumbani, huku matatu tu wakifunga ugenini, hivyo Simba nyumbani ni hatari zaidi.
Akizungumza na Mwanaspoti kwa njia ya simu kocha wa Al Masry Anis Boujelbene alisema, kikosi chake kinajiandaa na mchezo mgumu. Mtunisia huyo alisema; “Tupo kwenye maandalizi, tunaendelea kufanya kila tunalotakiwa ili tuwe tayari na mechi dhidi ya Simba, nafahamu tunakwenda kukutana na timu ngumu lakini kwetu tunatakiwa kuhakikisha tunafanya vizuri kwenye mchezo huu wa kwanza huku nyumbani.
“Tulijaribu kutafuta taarifa zao muhimu zipo baadhi tumezipata na zingine tumezikosa, lakini ukiangalia kikosi chao kwenye mechi za makundi utaona ni timu ambayo kama tukifanya makosa inaweza kufanya vizuri hata huku kwetu.”
Aidha Boujelbene alisema; “Tulikuwa tunaangalia wakiwa nyumbani unaona kabisa ni timu ambayo sio rahisi kupata ushindi ikiwa kwake,lakini kwetu tutajaribu kusawazisha hili bila kujali nguvu yao.”
“Wana kikosi imara sana kuna wachezaji kutoka Ivory Coast,Cameroon,Guinea na wengi wa Tanzania lakini wana ubora mkubwa na uzoefu wa kutosha, ni timu imara sana.”