Kumekuwa na matukio mengi ya utata katika mpira wa miguu , lakini hili limetokea kushtua wapenzi wengi wa soka kutokana na kile alichokizungumza kocha wa Club Brugge, Nicky Hayen baada ya kuweka wazi kuwa kabla ya mechi, huwa anazungumza na marehemu mama yake kama sehemu ya maandalizi jambo analoamini linampa nguvu na utulivu.
Akizungumza na waandishi wa habari kabla ya mchezo wao wa marudiano wa hatua ya mtoano ya Ligi ya Mabingwa dhidi ya Atalanta ambao Brugge imeshinda mabao 3-1, Hayen amesema tabia hiyo imemsaidia katika safari yake ya ukocha, hasa wakati akiiwezesha Brugge kushinda ubingwa wa Ubelgiji msimu uliopita.

“Daima huzungumza na mama yangu kabla ya mechi. Alifariki miaka minne iliyopita. Mwaka jana kabla ya hatua ya mchujo ya ligi ya Ubelgiji, nilimwambia tunataka kufanya jambo la kipekee, na mwishowe tukafanikiwa kushinda ubingwa,” amesema Hayen.
Hayen ameongeza kuwa yeye si mtu mwenye imani ya kidini kwa kiwango kikubwa, alieleza kuwa anaamini kuna nguvu fulani inayomsaidia.
Kocha huyo mwenye umri wa miaka 44 alijiunga na Club Brugge Machi mwaka jana kwa muda mfupi, lakini akaiongoza timu hiyo kubadilisha matokeo yao na hatimaye kushinda ubingwa wa Ubelgiji.
Kutokana na mafanikio hayo, alipewa mkataba wa kudumu Juni mwaka huu na sasa ameifikisha Brugge hadi hatua ya 16 bora ya Ligi ya Mabingwa Ulaya huku akiiweka timu yake katika nafasi ya pili kwenye msimamo wa Ligi Kuu ya Ubelgiji.
Baada ya ushindi wa mabao 3-1 dhidi ya Atalanta, Club Brugge sasa imefuzu kucheza katika hatua ya 16 bora ya Ligi ya Mabingwa Ulaya kwa ushindi wa jumla wa mabao 5-2 ambapo mechi ya kwanza ilishinda mabao 2-1 ikiwa nyumbani Ubelgiji na ikashinda mabao 3-1 jana Italia.

Timu itakayokutana na Club Brugge katika hatua ya mtoano ya 16 bora ijipange mapema kabla ya kocha Nicky Hayen hajaenda kuongea na mama yake.