KMC haijafanya kosa kikanuni kwenda Tabora

Kumekuwa na maoni tofauti juu ya uamuzi wa timu ya KMC kuamua kupeleka mchezo wake wa Ligi Kuu dhidi ya Simba, Mei 11 mwaka huu katika Uwanja wa Ali Hassan Mwinyi Tabora badala ya kuicheza katika Uwanja wake wa KMC Complex uliopo Mwenge, Dar es Salaam.

Wapo ambao wameiunga mkono KMC kwa kuamua hivyo lakini kuna ambao wanaonekana kuikosoa timu hiyo kwa kuamua mechi yake iwe Tabora badala ya kucheza katika uwanja wake wa siku zote ambao imeuzoea.

New Content Item (1)

Kila upande una hoja zake lakini mwisho wa siku KMC haijafanya kosa lolote la kikanuni kwa kufanya uamuzi huo hivyo hilo linafanya wawe sahihi kulingana na sababu ambazo wamezitaja na hata nyingine ambayo hawajaitaja lakini ina mashiko na imekuwa ndio chachu ya timu nyingi kuchukua uamuzi unaofanana na huo.

KMC wametaja sababu ya kwanza kuwa ni kuruhusiwa kikanuni kufanya hivyo kwa vile katika kanuni za Ligi Kuu msimu huu, ipo ambayo inazipa ruhusa timu kucheza mechi zisizozidi mbili katika Uwanja uliopo mwingine tofauti na ule wa kawaida ambao inautumia kwa mechi zake za nyumbani.

“Timu ya Ligi Kuu inaweza kuteua viwanja vingine miongoni mwa viwanja vilivyokaguliwa na kukidhi vigezo vya kikanuni kutumika kwa michezo ya Ligi Kuu kwa michezo yake miwili tu ya nyumbani na kuwasilisha uteuzi wake huo siku ishirini na moja (21) kabla ya mchezo husika inayokusudia kucheza kwenye uwanja wa uteuzi.

“Masharti ya uwasilishaji yatazingatia pia kanuni ya 9:3 ya Kanuni hizi. Uwanja ukishapitishwa hautabadilishwa isipokuwa kwa mazingatio ya Kanuni ya 9:6,” inafafanua kanuni

ya 9(7) ya Ligi Kuu 2024/2025.

Sababu nyingine ambayo KMC imeitaja ni ya kiufundi kwamba siku mbili baada ya mchezo dhidi ya Simba watakuwa na mechi ya ugenini dhidi ya Tabora United katika Uwanja huohuo wa Ali Hassan Mwinyi.

KMC wanaamini kwamba wakicheza mechi Dar es Salaam, wachezaji wao watachoshwa na umbali wa safari ya kwenda Tabora kwani watakuwa na muda mfupi wa kupumzika kujiandaa na mechi dhidi ya Tabora United jambo ambalo linaweza kuwafanya wapoteze pointi kwenye mechi hiyo.

Mechi hiyo kuchezwa Tabora inaonekana inaweza kuwa na athari kwa Simba ambayo inakabiliwa na mechi ya kwanza ya fainali ya Kombe la Shirikisho Afrika dhidi ya RS Berkane ya Morocco ambayo itacheza ugenini.

Kuna wasiwasi kwamba Simba inaweza kuchelewa kwenda Morocco kwa vile hakuna ndege zinazoenda Tabora kila siku hivyo italazimika kutoka mkoani humo na kurejea Dar es Salaam, Aprili 13 hivyo inaweza kujikuta ikifika Morocco kati ya Aprili 14 au 15.

Vyovyote itakavyokuwa, hili la KMC kupeleka mechi yake dhidi ya Simba katika Uwanja wa Ali Hassan Mwinyi Tabora linatukumbusha haja na umuhimu wa kuipitia upya na ikibidi kuirekebisha kanuni hiyo ambayo inazipa mwanya timu kutumia uwanja mwingine tofauti na ule wake wa nyumbani.

Kama tunaamua msimu ujao iendelee kutumika basi iwe na angalizo la hali ya kidharura kama hii iliyotokea kwa Simba ili kulinda maslahi ya taifa kwa kutoziathiri timu zinazoshiriki mashindano ya kimataifa.

Mfano pindi timu iliyoamua kuchezea uwanja mwingine dhidi ya timu inayoshiriki mashindano ya kimataifa, basi ni lazima mechi hiyo ichezwe katika mji ambao utakuwa na uwanja wa ndege ambao utawezesha timu kusafiri mara baada ya mchezo kumalizika.

Kama inashindwa kufanya hivyo basi mamlaka inayosimamia ligi ipewe rungu la kulazimisha timu icheze katika uwanja wake inaoutumia kwa mechi nyingine.

Lakini pia kanuni hii inapaswa kuwa na kipengele cha kuibana timu mwenyeji ilipe angalau nusu ya gharama za usafiri kwa timu ngeni kwa vile kitendo cha kubadilisha uwanja kinakuwa na athari ya moja kwa moja kiuchumi kwa timu inayokuwa ugenini.

Mwanzoni mwa msimu timu zinatengeneza bajeti ya kujiendesha kwa msimu mzima ambayo tayari inakuwa imeshatenga kiasi ambacho itakitumia kwa mechi za ugenini kwa kuzingatia vituo ambavyo wapinzani wao watacheza mechi za nyumbani.

Kitendo cha katikati ya msimu timu kubadilisha uwanja maana yake kitalazimisha timu kuingia gharama za ziada ambazo hazikuwa katika bajeti yake na hilo linaweza kusababisha hasara aambayo inaweza kuiweka timu katika wakati mgumu.

Kwa sasa inaweza kuchukuliwa kuwa ni jambo la kawaida kwa vile mara nyingi timu za ugenini ambazo zinakutana na changamoto ya wenyeji wao kubadili uwanja wa mechi ni Simba na Yanga ambazo zinaonekana zinajimudu kiuchumi.

Siku inaweza kutokea timu ambayo haiko vyema kiuchumi ndio ikajikuta inatakiwa ikacheze ugenini katika mji wa tofauti na ambao iliutegemea, ikashindwa kufika kwenye kituo cha mchezo na kupelekea ipate adhabu ya kupoteza pointi.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *