Klabu tatu za Gofu kuchuana kesho ‘Coastal Open Inter – Club’

Na Winfrida Mtoi, Mtanzania Digital

Klabu tatu za gofu zinatarajia kuchuana katika mashindano ya Ukanda wa Pwani ‘ Coastal Open Inter – Club yatakalofanyika kwa siku moja kesho Ijumaa Aprili 5, 2025 kwenye viwanja vya Klabu ya Gofu Lugalo, jijini Dar es Salaam.

Mashindano hayo yanayodhaminiwa na benki ya CRDB, yatahusisha zaidi ya wachezaji 100 wa ridhaa na kulipwa kutoka klabu za Lugalo, Dar es Salaam Gymkhana na Morogoro.

Akizungumza na waandishi wa habari leo Aprili 4, 2025, Dar es Salaam Katibu wa Klabu ya Lugalo, Luteni Kanali Mstaafu Shabani Kitogo amesema mashindano hayo yanafanyika kwa mara ya tatu mfululizo yakidhaminiwa na benki hiyo.

“Maandalizi ya kiufundi yameshafanyika kinachosubiriwa ni wachezaji kuingia uwanjani, Napenda kuwakaribisha wanachama na wachezaji kuja kushiriki mashindano haya,” amesema.

Naye Mkuu wa Kitengo cha Wateja Binafsi wa CRDB, Stephen Adili amesema wamekuwa na ushirikiano mkubwa na uongozi klabu ya Lugalo na wataendelea kufanya hivyo kuhakikisha watanzania wengi wanashiriki michezo.

Adili amesema mchezo wa gofu ni kwa ajili ya rika zote bila kujali kipato cha mtu, hivyo kuwataka watu kujitokeza kwa wingi kushiriki katika michuano hiyo na kujifunza.

“CRDB tunatambua umuhimu wa michezo na tunashiriki sehemu nyingi kama vile kwenye baskeball, football na michezo mingine. Tunajua michezo lugha ya Kimataifa na sehemu ambayo watu watakutana na kuimarisha ushirikiano na undugu,”. amesema Adili.

Kwa upande wake Nahodha Msaidizi wa Klabu ya Lugalo, Samwel Mosha amesema watacheza katika mfumo wa mchezaji mmoja mmoja kila mchezaji akijipambania mwenyewe tofauti na mashindano yaliyopita.

“ Wachezaji watakaoshindana ni daraja A,B, C, wanawake na wazee. Zawadi kwa washindi zitakuwa ni fedha tasilimu na vitu. Tunaishukuru benki ya CRDB kwa jinsi wanavyoendelea kutushika mkono,” ameeleza.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *