
Mbeya. Pamoja na mchakato wa uchaguzi kuendelea kwa amani jijini hapa, baadhi ya wapiga kura wameeleza changamoto ya majina kutopangwa kwa mtiririko wa herufi (alfabeti), hali iliyosababisha ugumu kwa wazee na watu wenye uoni hafifu.
Mwananchi Digital imefika kwenye baadhi ya vituo vya kupigia kura jijini hapa leo Jumatano Novemba 27, 2024 na kushuhudia wananchi wakihakiki majina yao ili kutimiza haki yao ya kikatiba ya kupiga kura.
Aidha, wazee waliwekwa katika makundi maalumu kwa lengo la kupewa kipaumbele na kusaidiwa kuthibitisha majina yao.
Msimamizi Msaidizi wa Kituo cha Sinde B, Jijini Mbeya, Godfrey Andrew ameiambia Mwananchi kuwa majina kutokuwa kwenye mpangilio ni kutokana na mchakato wa kujiandikisha ulikuwa kila mpigakura alifikakwa wakati wake na ndivyo ilivyoandikwa vivyo hivyo.
Andrew amesema wazee na vikongwe wamepewa kipaumbele kwa lengo la kuhakikisha kila mmoja anapata haki yake ya kupiga kura.
“Wazee na vikongwe tunawapa kipaumbele sana, ndiyo maana tumewaweka sehemu maalumu ili kuwarahisishia kuhakiki majina yao na kupata namba kwa urahisi, hapa mtu akifika akishahakiki jina lake tunampa namba ya kuingia kupiga kura,” amesema Andrew.
Hata hivyo, Masage Mwambuma amesema mchanganyiko wa majina unawafanya watumie muda mrefu kuyatafuta hali inayosababisha baadhi ya wapigakura kukata tamaa na kuondoka.
“Majina ni mengi yako zaidi ya 900 na kuyatafuta bila mpangilio inachukua muda mwingi. Yangepangwa kwa alfabeti, ingerahisisha kazi hii,” amesema Mwambuma.
Naye Diana Fumbo amesema ugumu huo unawaathiri zaidi wazee na wenye uoni hafifu, hasa kutokana na maandishi yasiyoonekana vizuri.
“Kwa maandishi haya, mzee au mwenye uoni hafifu atapata changamoto kubwa. Utaratibu bora unahitajika,” amesema Diana.
Kwa upande wake, mgombea wa Chadema, mtaa wa Mtoni, Elisha Chonya amesema changamoto za awali, kama tatizo la karatasi, zilitatuliwa kwa busara na kazi ya upigaji kura inaendelea vizuri.
“Shughuli ilianza saa 2 asubuhi. Kulikuwa na changamoto ya karatasi ila ilitatuliwa haraka kwa sasa upigaji kura unaendelea kwa amani tu,” amesema Chonya.
Naye wakala wa CCM, Evans Kaimu amesema anaridhishwa na mchakato licha ya changamoto ndogondogo zinazojitokeza, lakini zinapatiwa ufumbuzi kwa haraka.
“Shughuli inaendelea kwa amani na kila mmoja anapata haki yake. Changamoto zilizojitokeza zimewekwa sawa,” amesema Kaimu.
Wananchi Geita wahoji
Baadhi ya wananchi katika Halmashauri ya Mji wa Geita, mkoani Geita, wamelalamikia mpangilio usio rafiki wa majina katika daftari la wapigakura, wakidai kutokuwekwa kwa alfabeti kunawafanya kutumia muda mrefu kuyatafuta.
Wakizungumza katika maeneo ya kupigia kura, wananchi hao wamesema changamoto hiyo imeathiri kasi ya upigaji kura, huku wengine wakihofia kuchelewa kukamilisha hatua hiyo.
Akijibu malalamiko hayo, Msimamizi Mkuu wa Uchaguzi Jimbo la Geita Mjini, Yefred Myenzi, amesema majina hayo yameorodheshwa kwa utaratibu wa jinsi watu walivyojiandikisha. Hata hivyo, amewataka wapiga kura kutulia na kutumia namba zao za usajili kama njia rahisi ya kuyapata majina yao.
“Kwa uchaguzi huu, utaratibu wetu ndio huu. Haya maoni yanayotolewa kwamba tupange majina kwa alfabeti tumeyachukua na yatafanyiwa kazi katika uchaguzi ujao. Ila watu watulie waangalie majina yote yapo,” amesema Myenzi.