Kiwango cha Samatta PAOK moto!

KWA kiwango anachoonyesha Mbwana Samatta katika Klabu ya PAOK kule Ugiriki ni kama kinawapa mtihani viongozi kuamua hatima yake kutokana na mkataba wake kukaribia mwisho.

Machi 2, mwaka huu, nahodha huyo wa Taifa Stas alifunga bao moja na asisti kwenye mechi ya raundi ya 25 dhidi ya Asteras Tripolis, PAOK ikiondoka na ushindi wa mabao 2-0 uliomfanya kufikisha mabao manne na asisti moja.

Samatta hakuwa na mwanzo mzuri wa msimu, lakini katika mechi tano mfululizo za mwisho alizocheza ameonyesha kiwango bora, hivyo akifunga tena atakuwa anazidi kuwapa mtihani viongozi kumuacha au kubaki naye baada ya msimu kumalizika.

Katika Ligi Kuu Ugiriki imebaki mechi moja ili ligi imalizike, lakini pia zimebakia mechi sita za ligi ndogo ili kumpata bingwa wa nchi hiyo atakayewakilisha katika Ligi ya Mabingwa Ulaya.

Ipo hivi; katika Ligi Kuu Ugiriki nafasi nne za juu bingwa hapatikani isipokuwa timu nne huanza kushindana upya na inayoshika nafasi ya kwanza na pili zinashiriki Ligi ya Mabingwa Ulaya ilhali mbili zinazoshika nafasi ya tatu na nne zinakwenda kucheza Europe League.

Endapo kama timu anayocheza Samatta ambayo kwa sasa ipo nafasi ya nne katika msimamo wa ligi hiyo ikifanikiwa kuchukua ubingwa, Mtanzania huyo atapata nafasi ya kucheza tena Ligi ya Mabingwa Ulaya kama msimu huu. 

Samatta ambaye ana rekodi kibao alizoweka akicheza soka nje ikiwamo kuibuka mchezaji bora wa Afrika na mfungaji bora wa KRC Genk ya Ubelgiji alikomaliza na mabao 20 msimu 2018/19, hivyo PAOK ikinyakua ubingwa atakuwa ameongeza rekodi zake.