
Dar es Salaam. Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) wa Tanzania, Charles Kichere ameyataja mashirika manne ya umma yaliyopata hati zenye shaka na hati mbaya katika ripoti yake ya mwaka wa fedha 2023/24.
Miongoni mwa mashirika hayo ni pamoja na kiwanda cha dawa cha Keko Pharmacetical kinachozalisha dawa na vifaatiba mbalimbali ikiwemo barakoa.
CAG ameyasema hayo leo Alhamisi, Machi 27, 2025 alipokuwa akiwasilisha ripoti yake ya ukaguzi kwa Rais Samia Suluhu Hassan ya mwaka wa fedha 2023/2024 Ikulu jijini Dar es Salaam.
“Taasisi zilizopata hati zenye shaka na hati mbaya ni pamoja na Kiwanda cha Dawa Keko, Bodi ya Chai Tanzania, Chuo cha Sukari cha Taifa na Shirika la Posta Tanzania haya ni mashirika ya umma,” amesema Kichere.
Katika upande wa miradi ya maendeleo, ameitaja Halmashauri ya Wilaya ya Arumeru, Mfuko wa Afya pia zilipata hati mbaya.