Kiungo Yanga Princess aahidi makubwa

KIUNGO wa Yanga Princess, Lydia Akoth amesema kuonyeshwa upendo na mashabiki wa timu hiyo inampa deni kubwa la kuipambania kuhakikisha inafanya vizuri kwenye mechi zilizosalia.

Nyota huyo raia wa Kenya alisajiliwa dirisha dogo msimu huu akitokea Kenya Police Bullents FC ya nchini kwao na ndani ya muda mchache amekuwa akizungumzwa na mashabiki wa timu hiyo wakimsifu kwa uwezo wake.

Akoth alisema licha ya ugeni kwenye Ligi ya Tanzania lakini amepokelewa kwa ukubwa akitoa pongezi kwa mashabiki wa timu hiyo kujitolea kuja uwanjani kuishabiki timu yao.

“Kama mchezaji inanipa hamasa kwa kiasi kikubwa kwa sababu hii ni mara yangu ya kwanza kucheza soka la kulipwa Tanzania, lakini unaona mashabiki wanavyokushangilia, inamaana wanakuamini, hivyo napambana kuhakikisha siwaangushi na kuendeleza pale tulipoishia,” alisema Akoth.

Akiwa Kenya Police alikuwa kiungo muhimu kwenye timu hiyo ambayo msimu wake wa kwanza aliisadia kuchukua ubingwa likiwa taji la kwanza kwa timu hiyo akifunga mabao nane na asisti 10 kwenye mechi 18.

Kiwango alichoonyesha kilimfanya anyakue tuzo ya mchezaji bora wa mwaka (MVP) mbele ya Maximilla Robie wa Kibera Queens na Rebecca Okwaro anayekipiga timu moja.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *