Kituo cha Polisi chafungwa kisa deni la Sh40.9 milioni ya pango

Kenya. Katika hali isiyo ya kawaida Kituo cha Polisi cha Riandira Kaunti ya Kirinyaga nchini Kenya kimefungwa kwa muda usiojulikana kutokana na malimbikizi ya deni la kodi ya Sh2 milioni ya Kenya (Sh40.9 milioni za Tanzania).

Televisheni ya Citizen nchini humo imeripoti leo Jumanne Machi 25, 2025, kuwa Kituo hicho kimekuwa kikiwahudumia wakazi wa eneo hilo kwa takriban miaka tisa katika jengo linalomilikiwa na mtu binafsi.

Kituo hicho kilifungwa Machi 24, 2025, huku uamuzi huo ukiwafanya wakazi wa Soko la Riandira na viunga vyake kujawa na hofu ya kiusalama. Polisi walionekana wakibeba virago vyao na kuondoka katika eneo kilipo kituo hicho jambo lililowashangaza wakazi hao.

“Maofisa hao wameondoka na hatujui walikokwenda, kwa kweli waliimarisha usalama katika eneo hili sasa tutateseka,” amesema Mkazi wa Kaunti hiyo, Grace Wanjiru.

Mwaka 2016, tajiri wa eneo hilo, marehemu, Mwangi Thuita alitenga jengo hilo kwa lengo la kuanzisha Kituo cha Polisi kutokana na  kuongezeka kwa matukio ya uhalifu na ukosefu wa usalama katika eneo hilo.

Polisi walipaswa kuendelea kulipa kodi ama kuondoka katika jengo hilo baada ya Serikali kujenga kituo chake cha Polisi katika eneo hilo.

Hata hivyo, Serikali haijajenga kituo chake cha Polisi na maofisa wake wa usalama waliendelea kufanya kazi kwenye jengo la kibinafsi bila kulipa chochote hadi tajiri huyo alipofariki mwaka  2018.

Lakini familia ya tajiri huyo ilichoka kuwavumilia maofisa hao wa polisi ndipo ilipofikia uamuzi wa kuwafukuza na kusababisha kufungwa kwa kituo hicho.

“Kabla ya baba yetu kufariki, alituambia kuwa maofisa waliokuwa katika kituo cha polisi walipe kodi. Maofisa hao waliendelea kumiliki jumba hilo bila kulipa kodi na ikabidi waondoke ili tukodishe jengo hilo kwa mtu mwingine,” alisema mtoto wa mmiliki wa eneo hilo, Irene Njeri,

Hofu kwa raia

Wakazi wa eneo hilo, wanahofia kuwa ukosefu wa usalama utarejea katika eneo hilo kwani maofisa wa usalama wamehamishwa baada ya kituo hicho kufungwa.

Kwa mujibu wa Wanjiru: “Kituo hicho kimekuwa muhimu kwetu, sasa tumeingiwa na hofu kwa sababu hakuna maafisa wa usalama wa kukabiliana na wahalifu, tangu kifunguliwe, tumekuwa tukiishi kwa amani na matukio ya uhalifu yalipungua lakini sasa huenda majambazi wakaanza kuvamia nyumba zetu na maeneo ya biashara.”

Aliiomba Serikali kuingilia kati na kujenga kituo cha polisi kitakachoimarisha usalama.

Kwa upande wake, Francis Gikongo, alisema: “Serikali inafaa kuharakisha na kuweka kituo kipya cha polisi katika eneo hilo kabla ya majambazi hawajaanza kututia hofu na kutuhangaisha.”

Imeandikwa na Mgongo Kaitira kwa msaada wa mashirika ya habari.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *