
Dar es Salaam. Staa wa Bongo Fleva, Zuchu yupo mbioni kuachia albamu yake mpya ya kwanza tangu ametoka kimuziki miaka minne iliyopita na kuna mengi ya kutarajia katika mradi huo ambao maandalizi yake yameanza muda mrefu.
Zuchu atakuwa msanii wa tatu wa WCB Wasafi kutoa albamu chini ya rekodi lebo hiyo baada ya Rayvanny, Sound From Africa (2021), Mbosso, Definition of Love (2021) na D Voice, Swahili Kid (2023).
Ataungana na wasanii wengine wa Bongo Fleva ambao tayari wametoa albamu kwa mwaka huu, wasanii hao ni Roma ‘Nipeni Maua Yangu’, Jay Melody ‘Therapy’, Harmonize ‘Muziki wa Samia’, Young Lunya ‘Mbuzi’, Stamina ‘Msanii Bora wa Hip Hop’ n.k.
Zuchu anakuja na albamu baada ya kufanya vizuri na EP yake, I Am Zuchu (2020) iliyotoka na nyimbo saba huku akiwashirikisha wasanii wawili tu, Mbosso na Khadija Kopa ambaye ni mama yake mzazi.
Je, tutarajie nini katika albamu hii ya Zuchu, mshindi wa Tuzo saba za Muziki Tanzania (TMA) kwa misimu miwili tofauti?, haya ni mambo matatu ya kugojea.
Mosi; kolabo za kimataifa, tayari Zuchu amethibitisha kuwa Yemi Alade kutokea Nigeria ambaye amechaguliwa kuwania tuzo za 67 za Grammy katika kipengele cha ‘Best African Music Perfomance’ atakuwepo katika albamu hiyo.
“Hongera Malkia kwa kuchaguliwa kuwania tuzo za Grammy, asante kwa kuibariki albamu yangu kwa kipaji chako. Tuna mteule wa Grammy katika albamu yetu,” aliandika Zuchu kupitia Insta Story wakati akimpongeza Yemi.
Yemi Alade ambaye ni msanii wa kwanza wa kike Afrika kufikisha ‘views’ milioni 100 YouTube, tayari amefanya kazi na baadhi ya wasanii wa Tanzania akiwemo Harmonize aliyempa shavu katika wimbo wake, Show Me What You Got (2019).
Hata hivyo, hii itakuwa sio mara ya kwanza kwa Zuchu kushirikiana na msanii kutokea Nigeria, alishafanya kazi na wasanii wa huko kama Joeboy (Nobody), Olakira (Sere) na Adekunle Gold (Love).
Tunaamini albamu hii ya Zuchu itakuwa na wasanii wengi wa kimataifa maana WCB Wasafi mara zote wamefanya hivyo, mathalani albamu ya Mbosso iliwashirikisha Spice Diana (Uganda) na Liya (Nigeria) aliyesainiwa Davido Music Worldwide (DMW).
Pili; namba kubwa za mauzo, ni wazi albamu hii ya Zuchu atapata namba kubwa na kushika chati mbalimbali katika majukwaa mengi ya kidijitali ya kusikilizia na kuuza muziki, kama aliweza kufanya hivyo mwaka 2020, sasa itakuwa zaidi yake.
Ikumbukwe EP yake, I Am Zuchu (2020) ambayo imesikilizwa (streams) mara milioni 33.2 Boomplay Music, ilikaa tano bora kwenye chati za Boomplay Album kwa wiki 75, huku ukishika namba moja kwa wiki 35.
Pia EP hiyo ilimfanya Zuchu kuwepo katika chati za YouTube Music Tanzania kwa wiki zaidi ya 100 na ndiye msanii wa kike Bongo aliyekaa kwenye chati hizo kwa muda mrefu zaidi, huku akiwa wa kwanza Afrika Mashariki kufikisha ‘views’ milioni 100.
Hayo alifanya miaka minne iliyopita, vipi itakuwaje sasa ambapo tayari amejenga himaya yake katika Bongo Fleva akiwa ameshinda tuzo zaidi ya 10?, ni wazi ataweka rekodi nyingi za namba kubwa za mauzo.
Kufanya vizuri kwa albamu hiyo, huenda naye akashinda tuzo ya TMA katika kipengele cha Albamu Bongo 2024 akipokea kijiti hicho kutoka kwa Alikiba – Only One King (2021), Barnaba – Love Sounds Different (2022) na Harmonize – Visit Bongo (2023).
Tatu; kolabo na Diamond Platnumz, hili ni jambo ambalo haliepukiki kivyovyote vile na kama isipokuwa hivyo maswali yatakuwa mengi maana hakuna albamu ya msanii yeyote wa WCB Wasafi iliyowahi kutoka bila Diamond kushirikishwa.
Mathalani albamu ya mwisho kutoka chini ya WCB Wasafi ni yake D Voice, Swahili Kid (2023), Diamond alishirikishwa katika wimbo namba tisa, kama wengine.
Ukiachana na sababu hiyo, pia Diamond na Zuchu muunganiko wao wa kikazi umekuwa na matokeo mazuri ndio maana wamefanya kazi nyingi pamoja, tayari wametoa nyimbo nne, Cheche (2020), Litawachoma (2020), Mtasubiri (2022) na Raha (2024).
Tangu kumsaini Zuchu ndani ya WCB Wasafi mwaka 2020, Diamond hajafanya kolabo na msanii yeyote wa kike Tanzania!, ni yeye na Zuchu tu, vipi akosekana katika albamu yake tena ya kwanza?, hilo haliwezekani.
Ikumbukwe Zuchu anaenda kutoa albamu wakati Lady Jaydee akiwa msanii wa kike Bongo aliyetoa albamu nyingi ambazo ni nane, kwa ujumla ni wa pili baada ya Sugu (10), kisha Nikki Mbishi (7), Harmonize (5) Soggy Doggy (5), Juma Nature (5) na Professor Jay (4) n.k.