Kisukari kinavyosababisha matatizo ya mfumo wa mkojo

Kiwango kikubwa cha sukari mwilini kinaweza kuathiri baadhi ya viungo au mfumo mzima wa utendaji kazi wa mwili, hii ni pamoja na mishipa ya neva na damu. Hali hii inaweza kusababisha matatizo mbalimbali ya kiafya, ikiwemo matatizo ya mfumo wa mkojo.

Mfumo wa mkojo unajumuisha figo, kibofu cha mkojo, urethra na ureta ambao ni mrija unaopeleka mkojo kutoka kwenye figo hadi kibofu cha mkojo na urethra ni mrija unaopeleka mkojo nje ya mwili.

Kisukari kinapoharibu mfumo huu wa mkojo, kinaweza kusababisha matatizo kama vile shida ya kibofu cha mkojo, maambukizi ya njia ya mkojo na hata ugonjwa wa figo.

Tatizo moja linaloweza kuathiri watu wenye kisukari ni utendaji duni wa kibofu cha mkojo. Kibofu hushindwa kufanya kazi vizuri kama inavyopaswa. Kama sukari ikiwa juu kiwango kwa muda mrefu, inaweza kuharibu neva zinazosaidia kudhibiti kibofu cha mkojo.

Hali hii kitaalamu ni ‘Diabetic Cystopathy’. Hali hii husababisha mgonjwa wa kisukari kutohisi kibofu chake kikiwa kimejaa na anaweza kwenda chooni mara chache na mkojo unakaa kwenye kibofu kwa muda mrefu.

UTI inaweza kudhoofisha mfumo wa kinga na kufanya iwe vigumu kwa mwili kupambana na maambukizi.

Ikiwa sukari imeathiri njia ya mkojo kwa muda mrefu na mkojo unakaa kwenye kibofu kwa muda mrefu, bakteria wanaweza kukua na kuongeza hatari ya kupata UTI.

Maambukizi ya UTI yasipotibiwa yanaweza kuenea hadi kwenye figo na kusababisha maambukizi makali zaidi. Ni muhimu kwa watu wenye kisukari kufahamu dalili za UTI na kutafuta msaada wa daktari wanapoona dalili za maambukizi.

Dalili za UTI ni kama kuhisi maumivu wakati wa kukojoa, kuwa na uhitaji wa haraka wa kukojoa au mkojo wenye rangi au harufu mbaya.

Kudhibiti viwango vya sukari ni moja ya njia bora za kuzuia uharibifu wa neva na mishipa ya damu. Hii inaweza kupunguza hatari ya matatizo ya mfumo wa mkojo. Kunywa maji ya kutosha husaidia kusafisha bakteria kwenye mfumo wa mkojo na kupunguza hatari ya maambukizi.

Kufanya uchunguzi na vipimo mara kwa mara ili kufuatilia afya ya figo. Kipimo rahisi cha mkojo au damu kinaweza kusaidia kugundua dalili za mapema za matatizo ya figo.

Epuka uvutaji sigara na pombe. Kuvuta sigara na matumizi makubwa ya pombe kunaweza kuharibu figo na kibofu cha mkojo na kuongeza hatari ya matatizo ya kiafya.