
Marekani, Rais akiwa Joe Biden, Urusi na Vladimir Putin, Ukraine na Volodymyr Zelenskyy, taswira ya mapambano ya vita ya Urusi-Ukraine, ilikuwa mithili ya Mexican Standoff, mchuano hatari kila upande.
Mexican Standoff, hutokea kwenye mapigano yenye kushirikisha bunduki. Kila upande umemnyooshea mwenzake silaha, hakuna mkakati salama wa ushindi kwa yeyote. Ukifyatua, na mwenzako anapiga, hatari kwa wote.
Vita ya Urusi-Ukraine, ilikuwa sawa na Mexican Standoff ya pande tatu; Urusi ilinyoosha silaha kwa Ukraine, ambayo nayo ilijibu mapigo, kisha Marekani na Ulaya, wakasimama na Ukraine, kuitisha Urusi. Hali hiyo ilisababisha kila upande uwe na hofu.
Haijatimia miezi miwili tangu Donald Trump, ale kiapo kuwa Rais wa Marekani kwa muhula mwingine, akipokea kijiti kutoka kwa Biden. Hali ya vita ya Urusi-Ukraine imebadilika. Marekani ya Trump, imeunda “ushosti” usioeleweka na Urusi, sasa Mexican Standoff ni Ukraine dhidi ya Urusi na Marekani.
Februari 28, 2025, kasheshe ilitokea ndani ya ofisi binafsi ya Rais wa Marekani (The Oval Office) na kuifanya Ikulu ya Marekani, White House, iandike rekodi ya aina yake. Zelenskyy alisafiri kutoka Kyiv hadi Washington DC umbali wa kilometa 8,759 au maili 5,443, kufanya mazungumzo na Trump.
Pengine, alikuwa na matarajio chanya. Hata hivyo, mwenzake, Trump, alishaandaa mpango wa kumpa joto ya jiwe. Kwanza, mkutano ulikuwa wa faragha baina ya viongozi hao wawili wa nchi mbili tofauti, Trump na menejimeti ya White House ikahakikisha vyombo vya habari vinakuwepo na kurekodi mazungumzo yote.
Mazungumzo yaliwahusu marais wawili, Trump na Zelenskyy, lakini Makamu wa Rais wa Marekani, JD Vance, alikuwepo na akawa wa kwanza kumchokonoa Zelenskyy. Mwisho, Zelenskyy akajikuta kawekwa mtu kati. Akigeuka Trump anamparura usoni, kabla ya hajajibu Vance naye anamshindilia.
Mazungumzo ambayo ni sahihi kuyaita mabishano ya Oval Office, yalijengwa na ushawishi wa misimamo ya kisasi, aliyonayo Trump dhidi ya Biden na Rais wa 44 wa Marekani, Barack Obama, vilevile hali ya Trump kujiona bora mbele ya marais wa nchi hiyo waliomtangulia.
Mabishano ya Oval Office, yalikuwa na msukumo wa Trump, kutaka aonekane mwema kwa Putin, vilevile kuwaambia Wamarekani na dunia kuwa yeye (Trump) anaheshimiwa mno na Putin, hivyo ni rahisi kuelewana. Trump alisema katikati ya mabiashano ya Oval Office kwamba Putin hakuwaheshimu Biden, Obama na Rais wa 43 wa Marekani, George Bush, hivyo isingewezekana kufanya nao makubaliano. Trump alisema hivyo kwa kujiamini, alipokuwa akijibu swali la mwandishi, aliyehoji iwapo Putin atavunja makubaliano ya kusitisha mapigano na Ukraine.
Ukipitia neno kwa neno ubishi wa Oval Office, utagundua kuwa Zelenskyy amekuwa kondoo wa kafara, mawe yote aliyotupiwa ni kwa niaba ya Biden na Obama, lakini kwa umuhimu ni kumfurahisha Putin. Hayana masilahi kwa Wamarekani wala dunia.
Tuyaone malumbano
Vance alisema: “Kwa miaka minne, Marekani, tulikuwa na Rais aliyesimama kwenye mkutano na waandishi wa habari, akazungumza vibaya kuhusu Vladimir Putin, kisha Putin akaivamia Ukraine na kuharibu sehemu muhimu ya nchi.”
Akaendelea kueleza kuwa njia ya amani na ustawi ni ushirikishaji wa kidiplomasia. “Tulijaribu njia ya Joe Biden ya kujipiga kifua na kujifanya maneno ya Rais wa Marekani yana maana kuliko vitendo vya Rais wa Marekani.
Kinachoifanya Marekani kuwa nchi nzuri ni ushiriki wake kwenye diplomasia. NS hiki ndicho Rais Trump anafanya.”
Zelenskyy akaomba kuuliza swali, Vance alimkubalia, halafu Zelenskyy aliendelea: “Putin ameshikilia sehemu zetu, sehemu kubwa za Ukraine, sehemu za Mashariki na Crimea. Alitwaa maeneo hayo mwaka 2014. Hivyo, kipindi cha miaka mingi, siongelei kuhusu tu Biden, isipokuwa nyakati zote alipokuwepo Rais Obama, kisha Rais Trump, kisha Rais Biden na sasa Rais Trump.”
Zelenskyy akaendelea: “Mungu bariki, sasa, Rais Trump atamdhibiti. Lakini mwaka 2014, hakuna aliyemdhibiti, alitwaa na kushikilia. Aliua watu. Unajua nini…” Trump alimkatisha, akamuuliza, ilikuwa mwaka 2015? Zelenskyy akajibu: “Mwaka 2014.”
Trump akasema: “Mwaka 2014, mimi sikuwepo.” Vance akashadadia: “Hiyo ni kweli kabisa.”
Zelenskyy akajibu: “Ni kweli, lakini kutoka mwaka 2014 mpaka 2022, hali ipo vilevile, watu wamekuwa wakiuawa na jeshi lilelile, hakuna aliyemfanya aache. Unajua kwamba tulishakuwa na mazungumzo na yeye (Putin), mazungumzo mara nyingi.
“Tulishakuwa na mazungumzo ya nchi mbili. Na tukasaini naye, mimi, wewe (Trump) mwaka 2019, nilisaini naye makubaliano. Macron (Rais wa Ufaransa, Emmanuel) na Markel (Kansela wa zamani wa Ujerumani, Angela). Tulisaini kusitisha mapigano. Wengi wao waliniambia asingekwenda vitani. Lakini baada ya hapo, alivunja makubaliano ya kusitisha mapigano. Aliua watu wetu. Tulisaini kubadilishana wafungwa lakini hakutekeleza. Ni aina gani ya diplomasia unaizungumzia JD? Unamaanisha nini?”
Vance: “Nazungumzia diplomasia ambayo itamaliza uharibifu kwenye nchi yako. Bwana Rais, kwa heshima, nadhani ni utovu wa nidhamu wewe kuja Oval Office kujitahidi kubisha haya mambo mbele ya vyombo vya habari vya Marekani.
Sasa hivi, mnakwenda sehemu tofauti kujaribu kulazimisha kupata wanajeshi wa kusimama mstari wa mbele kwa sababu mna tatizo la nguvu kazi. Unatakiwa kumshukuru Rais (Trump), kwa kujaribu kulifanya hili suala lifike mwisho.”
Kutokana na maelezo hayo, Zelenskyy alimuuliza swali Vance: “Umewahi kuwepo Ukraine kwamba unasema hilo ndilo tatizo tulilonalo?”
Jibu la Vance lilikuwa wazi hajawahi kuwepo Ukraine, Zelenskyy akamwalika: “Uje hata mara moja.”
Hapo Zelenskyy aliweza kumwonesha Vance, kwamba Makamu wa Rais wa Marekani, alikuwa anajenga hoja kwa mtindo wa kukejeli na kukebehi wakati hali halisi haijui.
Vance alisema amekuwa akiona na kusoma habari. Akamuuliza kama hakuna tatizo la kuingiza watu jeshini.
“Tuna matatizo…, Zeleynskyyy alianza kujibu. Vance akamkatisha, akamwambia: “Unafikiri ni heshima kuja Oval Office na kuushambulia utawala ambao unajaribu kuzuia uharibifu kwenye nchi yako?”
Zelenskyy: “Maswali yamekuwa mengi sana, ngoja tuanzie mwanzo. Kwanza kabisa wakati wa Vita kila mtu ana matatizo, hata ninyi. Lakini mna bahari nzuri lakini hampati hisia nayo kwa sasa. Lakini mtapata hisia nayo siku zijazo. Mungu bariki…,” Trump alimkatisha.
“Hujui hilo. Usitwambie tutajisikiaje. Tunajaribu kutatua tatizo. Usitwambie tutajisikiaje.”
Zelenskyy: “Sikwambii wewe. Najibu haya maswali.
Trump: “Kwa sababu huna nafasi ya kulazimisha hilo.”
Vance: “Hicho ndicho hasa unachofanya.”
Trump: “Huna mamlaka yoyote ya kulazimisha vile ambavyo sisi tutajihisi. Tutajihisi vizuri sana.”
Zelensky: “Mtajihisi kushawishika.”
Trump: “Tutajihisi vizuri sana na imara sana.”
Zelenskyy: “Nakwambia, mtajihisi kushawishika.”
Trump: “Kwa sasa, haupo kwenye nafasi nzuri sana. Umeruhusu wewe mwenyewe kuwa kwenye nafasi nafasi mbaya sana.”
Zelenskyy: “Kuanzia mwanzo kabisa wa vita,” Trump akamkatisha, akamwambia: “Haupo kwenye nafasi nzuri. Hauna karata kwa sasa. Ukiwa na sisi, utaanza kuwa na karata.”
Zelenskyy: “Mimi sichezi karata. Nipo makini sana, Bwana Rais. Nipo makini sana.”
Trump: “Unacheza karata. Unacheza kamari na maisha ya mamilioni ya watu. Unacheza kamari na Vita Kuu ya Tatu ya Dunia.”
Zelenskyy: “Unazungumzia nini hasa?”
Trump: “Unacheza kamari na Vita Kuu ya Tatu ya Dunia. Na unachofanya ni utovu wa nidhamu mkubwa kwa nchi, hii nchi ambayo imekuwa ikikukingia kifua kwa kiwango ambacho watu wengi wanasema kimepitiliza.”
Vance akamuuliza Zelenskyy: “Umeshasema asante japo mara moja?”
Zelenskyy: “Mara nyingi. Hata leo.”
Vance: “Hapana, kwenye kikao hiki. Ulienda Pennsylvania Oktoba na kuufanyia kampeni upinzani.”
Zelenskyy: “Hapana.”
Vance: “Toa maneno ya shukurani kwa Marekani na rais ambaye anajitahidi kuilinda nchi yako.”
Zelenskyy: “Tafadhali. Unafikiri kwamba kama utaongea kwa sauti kubwa kuhusu vita, utakuwa ….,”
Trump: “Haongei kwa sauti kubwa. Haongei sauti kubwa, nchi yako ipo kwenye tatizo kubwa.”
Zelenskyy: “Naweza kujibu?”
Trump: “Hapana. Umeshazungumza sana. Nchi yako ipo kwenye tatizo kubwa.”
Zelenskyy: “Nafahamu. Nafahamu.”
Trump: “Hutashinda. Hushindi hii. Una nafasi nzuri ya kuibuka vizuri ukiwa na sisi.”
Zelenskyy: “Bwana Rais, tunakaa kwenye nchi yetu. Tupo imara. Tangu mwanzo kabisa wa vita, tumekuwa peke yetu. Na tunashukuru. Nilisema asante.”
Trump: “Kama usingekuwa na vifaa vyetu vya kijeshi, vita hii ingeisha ndani ya wiki mbili.”
Zelenskyy: “Ndani ya siku tatu. Nilisikia hivyo kutoka kwa Putin. Ndani ya siku tatu.”
Trump: “Labda chini ya hapo Itakuwa vigumu sana kufanya kazi kama hivi, nakwambia.”
Vance: “Wewe sema asante.”
Zelenskyy: “Nimeshasema mara nyingi, kwa watu wa Marekani.”
Vance: “Kubali kuna kutokukubaliana, na twende kufanyia kazi hayo mambo ya kutokukubaliana, kuliko kujaribu kupambana kwenye vyombo vya habari vya Marekani, wakati unakosea. Tunajua unakosea.”
Trump: “Lakini ona, nafikiri ni vizuri kwa watu wa Marekani kuona kinachoendelea. Nafikiri ni muhimu sana. Ndiyo maana nimeacha haya mazungumzo yaendelee kwa muda mrefu. Unapaswa kushukuru.”
Zelenskyy: “Nashukuru.”
Trump: “Huna karata. Unazikwa pale. Watu wanakufa. Unapungukiwa wanajeshi. Inaweza kuwa jambo zuri, halafu unatwambia, sitaki kusitisha vita.
Sitaki kusitisha vita, nataka kwenda, na nataka hivi. Tazama, kama unaweza kusitisha mapigano sasa hivi, nakwambia, unapata, hivyo risasi zitakoma na watu wako hawatauawa.”
Zelenskyy: “Bila shaka tunataka vita ikome. Lakini nilishakwambia, lazima kuwe na uhakikisho.”
Trump: “Unasema hutaki kusitisha mapigano? Nataka mapigano yakome. Kwa sababu utafanikiwa kusitisha mapigano haraka kuliko kuwa na makubaliano.”
Zelenskyy: “Uliza watu wetu kuhusu kusitishwa kwa vita, nini wanafikiri.”
Trump: “Hiyo siyo mimi. Hiyo inamhusu mtu anayeitwa Biden, ambaye siyo mtu mwenye maarifa.”
Zelenskyy: “Huyo ni rais wako. Alikuwa rais wako.”
Trump: “Samahani. Yule alikuwa na Obama, ambaye alikupa karatasi, na mimi nakupa mikuki. Nilikupa mikuki ya kuondoa vile vifaru vyote vya kijeshi.
Obama alikupa karatasi. Sentensi ni Obama alikupa karatasi, na Trump alikupa mikuki. Unatakiwa uwe na shukurani zaidi kwa sababu ngoja nikwambie, huna karata. Ukiwa na sisi utakuwa na karata, bila sisi, huna karata yoyote.”
Mwandishi anauliza swali ambalo Vance analirejea kuwa itakuwaje endapo Urusi itavunja mkakubaliano ya kusitisha mapigano?”
Trump akajibu: “Nini, ikiwa chochote? Vipi kama bomu likidondokea kichwani kwako sasa hivi? Sawa, vipi kama watavunja? Sijui, walivunja kwa Biden kwa sababu Biden hakumheshimu (Putin). Hawakumheshimu Obama. Wananiheshimu mimi.”
Gharama ya kisasi
Mwaka 2019, Trump akiwa Rais wa Marekani, alinusurika kuondolewa madarakani baada ya kushitakiwa kwa makosa mawili; mosi ni matumizi mabaya ya ofisi, pili kulizuia bunge kufanya kazi zake. Msingi wa kesi hiyo ni Trump na Zelenskyy. Kuelekea Uchaguzi wa Rais Marekani 2020, Trump alimwomba Zelenskyy na viongozi wa mataifa mengine, watoa taarifa ambazo zingemdidimiza Biden, ambaye ndiye alikuwa mshindani wake.
Zelenskyy aliposhindwa kutoa taarifa mbaya kuhusu Biden, bila kuchelewa Trump alisitisha msaada ya dola 400 (Sh1.04 trilioni). Alimwambia kama alihitaji msaada, basi atoe taarifa hasi dhidi ya Biden. Alitaka iwe nipe nikupe.Trump anakumbuka jinsi Zelenskyy alivyogoma kumpa ushirikiano, matokeo yake chupuchupu aondolewe ofisini. Ukijumlisha na roho ya kisasi dhidi Biden na Obama, ni sababu Zelenskyy anapitia kipindi kigumu. Marekani inataka kusaini ‘dili’ la madini na Ukraine. Trump, anadhani kwa kutumia njia ya vitisho, yeye na Vance, mbele ya vyombo vya habari vya Marekani, wangeweza kumfanya Zelenskyy awe mpole na aogope, hivyo kunyenyekea na kusaini haraka.Trump haamini mafanikio kwa njia ya ushawishi anataka ubabe na kudhalilisha. Alitaka dunia nzima imwone Zelenskyy kituko, matokeo yake, alikosa fursa ya kifikia hatua ya kusaini biashara ya madini. Miaka yote, tangu Vita Kuu ya Kwanza ya Dunia, Marekani ilijijenga kupitia ushirika na Ulaya. Msimamo wa sasa wa Trump dhidi ya Zelenskyy na Ukraine, unasababishia Marekani na Umoja wa Ulaya, vilevile mshirika wake mkuu, UK, watazamane tofauti. Hii inakwenda kuidhoofisha Marekani. Wakati Trump alipokuwa Rais, muhula wake wa kwanza, Januari 20, 2017 hadi Januari 20, 2021, Obama alipata kusema, Trump huongoza nchi kama mchezo wa maigizo ya televisheni. Hata mkutano wa Zelenskyy The Oval Office, ilikuwa reality show.