Kisa Bellingham, Real Madrid yatishia kuhama La Liga

Real Madrid imeripotiwa kuwa na mpango wa kujitoa katika Ligi Kuu ya Hispania ‘La Liga’ na kutimkia kwingine kwa kile kinachotajwa ni kutotendewa haki na marefa wa ligi hiyo.

Uamuzi huo wa Real Madrid unatajwa kuchochewa na kitendo cha mchezaji wake Jude Bellingham kuonyeshwa  kadi nyekundu katika mchezo wa La Liga dhidi ya Osasuna, Jumamosi, Februari 15, 2025.

Katika mchezo huo ambao ulimalizika kwa sare ya bao 1-1, Bellingham alionyeshwa kadi hiyo nyekundu na refa Jose Luis Munuera baada ya kucheza faulo na kutukana.

Bellingham anadai kuwa refa alimaanisha vingine baada ya yeye kutoa kauli iliyotafsiriwa na refa Munuera kuwa ni tusi huku mchezaji mwenyewe akidai alitoa kauli ya kuashiria kutokuwa sawa yeye binafsi.

Na tukio hilo linatajwa kuikasirisha Real Madrid ambayo inaripotiwa kuwa inafikiria kuhama La Liga na kutua katika Ligi mojawapo kati ya mbili kubwa Ulaya.

Ligi hizo ambazo Real Madrid inafikiria kuhamia ni ama Ligi Kuu ya Italia ‘Serie A’ au Ligi Kuu ya Ujerumani ‘Bundesliga’

Hata hivyo Real Madrid italazimika kufanya kazi ya ziada ili kukamilisha jambo hilo kama itaamua kulivalia njuga kwa vile kukamilika kwake kunahitaji baraka kutoka taasisi mbalimbali Ulaya na duniani.

Kwanza itatakiwa ipate uthibitisho na ruhusa kutoka Shirikisho la Mpira wa Miguu Duniani (Fifa), Umoja wa Vyama vya Soka Ulaya (Uefa) na ligi ambayo klabu hiyo itaamua kuhamia.

Muda mfupi baada ya kadi nyekundu ya Bellingham, Real Madrid ilitoa taarifa ya kulalamika juu ya ambacho kimetokea.

“Kilichotokea kwenye Uwanja wa RCDE kinawakilisha kilele cha mfumo wa waamuzi ambao haukubaliki kabisa, ambapo maamuzi dhidi ya Real Madrid yamefikia kiwango cha ghiliba na upotoshaji wa mashindano ambayo hayawezi kupuuzwa tena.”

“Kwa kuzingatia uzito wa kilichotokea, Real Madrid inaitaka RFEF (Shirikisho la Mpira wa Miguu Hispania kukabidhi mara moja rekodi za sauti za VAR zinazohusiana na michezo miwili muhimu ya mechi hiyo:

“1. Rekodi za sauti za mawasiliano kati ya VAR na mwamuzi wa uwanjani katika hatua ya mchezaji Carlos Romero kumkabili Kylian Mbappé.2. Rekodi za sauti za mawasiliano kati ya VAR na mwamuzi wa uwanjani katika mchezo wa bao lililokataliwa la Vinicius Jr.

3. Mazungumzo kati ya wanachama wa chumba cha VAR katika michezo yote miwili.,” ilisema taarifa ya Real Madrid

Muda mfupi baada ya kauli hiyo ya Real Madrid, rais wa LaLiga, Javier Tebas alijibu na kudai kuwa  klabu hiyo ilishindwakutoa suluhu mbadala katika mkutano wa hivi majuzi.

Kwa mujibu wa Marca, alisema: ‘Sikushangazwa hata kidogo na barua ya Real Madrid, kwani haisemi chochote tofauti na kile ambacho kituo chao cha televisheni kimekuwa kikirudia kwa muda mrefu.

“Wengi wetu tunatetea mabadiliko makubwa katika mfumo wa usuluhishi, tukisogea karibu na mtindo wa Kiingereza au Kijerumani, na shirika tofauti kabisa na uwazi zaidi katika maamuzi yote ya kimuundo ya usuluhishi wa Uhispania,” alisema Tebas

Wakati huohuo, baada ya kutolewa nje kwa kadi nyekundu Jumamosi alasiri, Bellingham sasa anakabiliwa na uwezekano wa kufungiwa mechi 12 kufuatia maoni yake ya X dhidi ya mwamuzi.