Kisa Barcelona, UEFA yabadili mwamuzi fainali Inter, PSG

Shirikisho la Soka Barani Ulaya (UEFA) limempa adhabu Szymon Marciniak mwamuzi aliyechezesha mechi ya mkondo wa pili ya nusu fainali ya Ligi ya Mabingwa Ulaya iliyofanyika kwenye Uwanja wa Giuseppe Meazza kati ya waliokuwa wenyeji wa mchezo huo Inter Milan ambayo iliibuka na ushindi wa mabao 4-3 dhidi ya Barcelona, akinyimwa mechi ya fainali.

Awali mwamuzi huyo alikuwa ameshatangazwa kuwa ndiye atachezesha fainali ya Ligi ya Mabingwa kati ya PSG na Inter Milan Mei 31 nchini Ujerumani, lakini sababu ya makosa hayo ametupwa nje

Mwamuzi Marciniak aliyechezesha mchezo huo alikosolewa na kocha wa Barcelona, Hansi Flick kwa kutochezesha mchezo kiungwana akionekana kuipendelea zaidi Inter Milan katika maamuzi yake hususani katika mkwaju wa penalti aliowapa wapinzani wao ambapo kwa upande wao hakuonekana kufanya hivyo.

Katika mchezo huo ambao ulimalizika kwa Barcelona kuondolewa kwenye mashindano hayo kwa jumla ya mabao 7-6, lawama nyingi zilielekezwa kwa refa huyo.

Inter Milan ilikuwa ya kwanza kupata mabao mawili yaliyofungwa na nahodha wake Lautalo Martinez katika dakika ya 21 akimalizia pasi ya Denzel Dumfries huku bao la pili likifungwa na Hakan Çalhanoğlu kwa mkwaju wa penati mwishoni mwa kipindi cha kwanza.

Barcelona ilitoka nyuma ikichomoa mabao yote mawili yaliyofungwa na Eric Garcia katika dakika ya 54 na Dan Olmo ambaye alifunga la kusawazisha katika dakika ya 60 huku bao la tatu likifungwa na Raphinha katika dakika ya 87.

Kabla ya mchezo huo kumalizika Inter walipata bao la kusawazisha kupitia kwa Francesco Acerbi ambaye alimalizia pasi ya Denzel Dumfries kabla ya Davide Frattesi kufunga la nne katika muda wa ziada lakini kulikuwa na malalamiko kutoka kwa upande wa Barcelona wakidai kwamba kabla ya kufungwa kwa bao hilo ilionekana Denzel Dumfries akimchezea faulo beki wao Gerard Martín kosa ambalo waamuzi hawakulifanyia kazi.

Licha ya kuwa ndiye aliyekuwa amepangwa kuchezesha mechi ya fainali kati ya Inter Milan na PSG itakayofanyika Mei 31, mwaka huu Marciniak amekosa fursa hiyo na badala yake, mwamuzi kutoka Romania, Istvan Kovacs, ameteuliwa kuchezesha fainali hiyo. Kwa mujibu wa ripoti kutoka katika jarida la michezo la Hispania, Sport, uamuzi huu umechagizwa kutokana na kiwango kibovu cha uchezeshaji wake kwenye Uwanja wa San Siro.

Ripoti hiyo inabainisha kuwa maamuzi kadhaa ya utata yaliyofanywa na Marciniak wakati wa mchezo wa nusu fainali mengi kati yake yakiwaacha mashabiki na viongozi wa Barcelona wakiwa na hasira ndiyo yaliyomgharimu nafasi ya kuchezesha fainali hiyo kubwa. Adhabu ya penalti dhidi ya Pau Cubarsí na makosa yanayodaiwa kufanyika katika bao la kwanza na la tatu la Inter Milan, yalitajwa kuwa sababu kubwa zilizomletea matatizo mwamuzi huyo kutoka Poland.

Kutokana na hilo, Marciniak hatahusika pia katika fainali za Europa League wala Conference League, ambapo Felix Zwayer na Irfan Peljto wamepangiwa kuzichezesha fainali hizo.

Marciniak mwenye umri wa miaka 44, aliweka rekodi ya kuchezesha mchezo wa fainali ya Kombe la Dunia la mwaka 2022 lililofanyika Qatar ambapo Argentina waliibuka mabingwa kwa kuifunga Ufaransa kwa mikwaju ya penalti 4-2 baada ya sare ya mabao 3-3.

Mwamuzi huyu pia ndiye aliyechezesha mechi ya fainali ya Ligi ya Mabingwa Ulaya mwaka uliopita iliozikutanisha Real Madrid ambao walitwaa ubingwa huo kwa kupata ushindi wa mabao 2-0 dhidi ya Borussia Dortmund kwenye Uwanja wa Wembley, London.

Refa huyu amechezesha jumla ya michezo 674 ambapo katika michezo hiyo ameonyesha jumla ya kadi 2899 katika kadi hizo za njano ni kadi 2825 na nyekundu ni 74 wakati akitoa mikwaju ya penalti 286.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *