Mbeya. Ukosefu wa maabara na vifaa vya kisayansi vimetajwa kupunguza idadi ya wanafunzi wa masomo ya sayansi huku Serikali ikiombwa kuongeza nguvu ili kupata wataalamu wenye ujuzi kwa maisha ya sasa na ya baadaye.
Kauli hiyo imetolewa jana Ijumaa Mei 16, 2025 na wanafunzi wa Shule ya Sekondari Ivumwe ya jijini Mbeya wakati wa ziara ya kamati ya siasa ya Mkoa huo kutembelea miradi mbalimbali ya maendeleo mkoani humo na kuzungumza na wananchi kusikiliza kero.
Mwanafunzi Magdalena Wilson anyesoma kidato cha tatu shuleni hapo, amesema masomo ya sayansi yanahitaji zaidi vitendo, hivyo bila kuwa na vifaa somo hilo linaweza kuwa gumu na kufanya wanafunzi kulikimbia.

Amesema kwa sasa wanaishukuru serikali na uongozi wa shule hiyo namna walivyoweza kujenga maabala ya kisasa inayochochea mwanafunzi kusoma kwa ufanisi na kuwa na ndoto.
“Bila maabara yenye vifaa na vyenye ubora na kisasa somo la sayansi haliendi, hata wanafunzi wanaweza kukimbia somo husika, huku asilimia kubwa ni vitendo na matarajio yetu ni kufaulu kwakuwa mazingira yanaruhusu,” amesema Magdalena anayesoma tahasusi ya Fizikia, Kemia na Bailojia (PCB).
Naye Efron Chengula amesema ili kutengeneza wataalamu wenye uwezo na ujuzi kwa maisha ya sasa na ya baadaye serikali isaidie shule kupatikana kwa maabara na vifaa kwa wanafunzi wa masomo ya Sayansi.
Amesema Shule ya Ivumwe imekuwa na matokeo mazuri kutokana na uongozi kutambua umuhimu wa somo hilo kwa kwamba matarajio yake ni kuwa daktari bingwa wa upasuaji.
“Tunashukuru uwapo wa maabara hii ya kisasa, awali tulikuwa na ambayo imechakaa hali iliyotia hofu katika kufanikiwa kwenye masomo yetu na sasa tunaamini kufikia ndoto zetu,” amesema Wilson wa tahasusi ya Fizkia, Kemia na Hesabu (PCM).

Mkuu wa Shule hiyo, Oscar Mwaihabi amesema shule hiyo imekuwa na matokeo mazuri kwani mwaka 2024 kidato cha sita kimekuwa na ufaulu wa daraja la kwanza na pili pekee, huku kidato cha nne kikiwa na daraja la kwanza hadi tatu.
Kuhusu ujenzi wa maabara hiyo, Mwaihabi amesema hadi kukamilika kwake kutagharimu Sh157 milioni ambapo hadi sasa tayari Sh 141 milioni sawa na asilimia 89 huku ikihitajika Sh16.7 milioni na kwamba kukamilika kwake kutachochea zaidi ufaulu.
“Tunashukuru bodi na uongozi mzima wa Shule kwa namna wanavyojitolea katika shule hii pamoja na wadau waliotusapoti, hadi sasa maabara hii ya kisasa imegharimu Sh141 milioni huku gharama yake jumla ikiwa ni Sh 157 milioni,” amesema Mwaihabi.
Mjumbe wa Mkutano wa Chama Cha Mapinduzi CCM Mkoa wa Mbeya, (MNEC), Ndele Mwaselela amewaasa wanafunzi kumtanguliza Mungu katika masomo yao pamoja na kuweka nidhamu ili kutimiza ndoto zao.
“Yeyote aliyefanikiwa ameanza na Mungu, lakini nidhamu nzuri kwa kumuheshimu mwenzake, nawasihi zingatieni hayo mambo mawili ili muweze kutimiza ndoto zenu mfikie kiwangu chetu,” amesema Mwaselela.
Mwenyekiti wa chama hicho Mkoa wa Mbeya, Patrick Mwalunenge amewatoa hofu watumishi wa shule hiyo kuwa wataendelea kuwatetea pale wanapoingiliwa kwenye majukumu yao, akiwataka kuzingatia kanuni, miongozo ya Jumuiya ya Wazazi.
“Iwapo mtafanya majukumu yenu kwa kuzingatia miongozo ya Jumuiya tutawalinda, kwa kuwa kuna eneo hamfiki hivyo tutakuwa sauti zenu, lakini mkienda tofauti hatutakuwa upande wenu, naamini mmenielewa,” amesema.
“Niwapongeze kwa kazi nzuri mnayoifanya hadi kuwa katika ufaulu wa aina hii, ongezeni juhudi na CCM itakuwa pamoja na nyinyi kwakuwa tunaridhishwa na kazi yenu kwani wapo walimu wanaojichanga kwa ajili ya shule hii,” amesema Mwalunenge.