Dar es Salaam. Usiku wa Tuzo za Tanzania Comedy uliofanyika katika Ukumbi wa The Super Dome, Masaki, Februari 22, 2025, ulijaa hisia tofauti kwani washindi walisherehekea mafanikio yao baada ya kushinda katika vipengele mbalimbali huku wengine wakiondoka na huzuni baada ya kushindwa kupata tuzo.

Miongoni mwa waliotarajiwa kung’ara ni Kipotoshi, ambaye mashabiki wake waliweka matumaini makubwa katika vipengele vya ‘Best Male Stand Up Comedian of the Year’, ‘Best Comedy Special of the Year’, na ‘Best Comedian of the Year People’s Choice’. Hata hivyo, bahati haikuwa upande wake kwani licha ya kuwania tuzo tatu, hakufanikiwa kushinda yoyote.
Akizungumza na Mwananchi Digital muda mfupi baada ya tuzo hizo ambazo mgeni rasmi alikuwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan, Kipotoshi amesema ameyapokea matokeo kwa moyo wa utulivu na hana lawama zozote.
“Nimepokea vizuri tu kama unavyoniona sina manung’uniko. Kibinadamu kama hujajiandaa inaweza kukuumiza lakini kwangu kufika katika vipengele vitatu mbele ya Rais ni ushindi mkubwa sana. Tuzo ni bonasi tu.
“Mimi kwenye uzinduzi wa tuzo hizo baada ya kupewa nafasi kuongea kwa niaba ya wachekeshaji nakumbuka niliwaambia kuwa tuzo hizi inabidi utumie zaidi akili kuliko hisia kwa sababu zinaweza kukutoa kwenye mchezo, kwahiyo kama utatumia hisia zaidi itakupunguzia nguvu ya kufanya kazi.
“Kwahiyo nilikuwa nimeshajipanga zamani sana nipate nisipate haina shida, niko vizuri naweza kuhimili vitu vikubwa kuliko vidogo, unaweza kunipiga tukio ambalo utahisi nitalalamika lakini silalamiki, kisha kinaweza kuniliza kitu kidogo sana,” amesema Kipotoshi.

Amesema ilikuwa ndoto ya kila mchekeshaji kuonesha ujuzi wake mbele ya Rais na kwa upande wake imemuongezea kitu kikubwa sana, hata hivyo, mchekeshaji huyo amesema kwa hatua iliyofikia tasnia ya uchekeshaji kwa sasa anaiona mbali zaidi.
“Naiona mbali zaidi lakini pia itabidi hata sisi wachekeshaji au waandaaji wajue namna ya kufanya biashara. Maana yake ngoma ikivuma sana hupasuka, unajua hizi tuzo zimeanzia parefu sana kwasababu ndio tuzo za kwanza hata Tanzania Music Award hawajawahi kufanya hivi, kwahiyo tunaweza kufanya vizuri .

“Kama Rais alivyoongea kuwa jambo linapoanza kusapoti inaweza kuwa rahisi lakini kuendeleza ni ngumu kwahiyo tunatamani muendelezo wake uwe mzuri wa tuzo lakini pia kwa sisi upande wa sanaa tunapofanya Stand Up Comedy, wasiingie watu ambao watakuja kuharibu sanaa yetu, hilo ndio langu lakini naiona Comedy ikienda mbali zaidi,” amesema Kipotoshi.