
BODI ya Ligi Kuu Tanzania (TPLB) imetangaza tarehe mpya ya mchezo wa Ligi Kuu Bara kati ya Simba dhidi ya Dodoma Jiji.
Awali, mchezo huo uliahirishwa baada ya Dodoma Jiji kupata ajali ilipokuwa ikisafiri kutoka mkoani Lindi kuifuata Simba Dar es Salaam.
Kwa mujibu wa taarifa kutoka TPLB, mchezo huo sasa umepangwa kufanyika Machi 14, 2025, kwenye Uwanja wa KMC Complex jijini Dar es Salaam kuanzia saa 10:00 jioni.
TPLB imesisitiza kuwa uamuzi huo umezingatia hali ya afya ya wachezaji wa Dodoma Jiji, huku pia ikiheshimu haki za mashindano kwa kuhakikisha kila timu inapata nafasi sawa ya kushiriki.
Mashabiki wa soka nchini wanalivua pumzi pambano hilo kwa hamu, hasa kwa kuwa Simba inawania pointi muhimu katika mbio za ubingwa, huku Dodoma Jiji ikihitaji ushindi ili kujiondoa kwenye presha ya kushuka daraja.
Simba inashika nafasi ya pili kwenye msimamo wa ligi ikiwa na pointi 54 wakati Dodoma Jiji ni ya saba ikikusanya pointi 26, zote zikicheza mechi 21.
TPLB imewahimiza wadau wote wa soka, wakiwemo viongozi wa klabu na mashabiki, kushirikiana katika kuhakikisha mchezo unachezwa kwa hali ya amani na uungwana.
Tayari viongozi wa klabu zote mbili wamepewa taarifa kuhusu mchezo huo, na maandalizi yanatarajiwa kuanza mara moja ili kuhakikisha kila kitu kinakwenda sawa kabla ya tarehe ya mechi.
Wakati huohuo, bodi hiyo imewataka wadau wa soka kuendelea kufuatilia ratiba ya ligi kwa kuwa mabadiliko yanaweza kutokea kulingana na mazingira mbalimbali ya mashindano.