
KIPIGO cha mabao mabao 2-0 walichopata Fountain Gate juzi kutoka kwa Ken Gold kimeonekana kumchanganya kocha mkuu wa timu hiyo, Robert Matano huku akiifungia kazi beki yake akielekeza nguvu mechi yao na Kagera Sugar.
Matano ambaye alitambulishwa kikosini humo hivi karibuni akiziba pengo la mtangulizi wake, Mohamed Muya aliyesitishiwa mkataba kutokana na matokeo yasiyoridhisha.
Kocha huyo raia wa Kenya, alianza kibarua chake kwa sare ya bao 1-1 dhidi ya Simba na juzi akiwa ugenini jijini Mbeya alikumbana na kipigo hicho dhidi ya vibonde wa Ligi Kuu.
Timu hiyo inatarajia kuingia uwanjani Februari 14 kukiwasha dhidi ya Kagera Sugar, mchezo utakaopigwa Uwanja wa Kaitaba, mjini Bukoba ukiwa wa raundi ya 19 kwa timu hizo.
Matano alisema vijana hawakucheza vizuri haswa mabeki wake kuruhusu idadi hiyo ya mabao akieleza kuwa anaenda kusuka upya makali ili mechi dhidi ya Kagera Sugar, Februari 14 wafanye kweli.
Alisema bado ligi haijaisha na malengo yao ni kuona Fountain Gate inapambania nafasi nne za juu, akieleza makosa ya kiufundi atayafanyia kazi kuhakikisha wanafikia malengo.
“Hatukucheza vizuri kama nilivyotarajia, yapo makosa nimeyaona hasa eneo la beki lakini kabla ya mechi ijayo nitafanyia kazi ili kubaki kwenye malengo yetu,” alisema.
Alisema upinzani ni mkali kwenye ligi kwa kuwa kila timu inayo nafasi ya kushuka au kupanda nafasi kutokana na matokeo na atawaandaa vyema mastaa wake kuendeleza ubora.