
London, England. Baada ya kupokea kipigo cha bao 1-0 dhidi ya Tottenham, kocha wa Manchester United, Ruben Amorim amelalamika akisema kazi yake ni ngumu sana huku akitaja Ligi ya England kuwa na ushindani mkubwa.
Amorim ambaye alijiunga na United Novemba mwaka jana akichukua nafasi ya Erik ten Hag mpaka sasa ameiongoza United kushinda mechi nne, sare mechi mbili na kupoteza mechi nane katika mechi 14 za Ligi Kuu England.
“Kazi yangu ni ngumu sana, lakini niko hapa kuendelea na kazi yangu, nitajaribu kushinda tena mechi zinazofuata, hii ni Ligi ngumu zaidi duniani.” Amesema Amorim kocha wa Man United.
Kipigo cha jana dhidi ya Tottenham kilikuwa cha nane katika mechi 12 za mwisho ambapo United imeshinda mechi tatu na kutoa sare mechi moja.
Bao la Tottenham lilifungwa na James Maddison katika dakika ya 13 baada ya kumalizia mpira uliotemwa na kipa wa United, André Onana ambaye alipigiwa shuti na Lucas Bergvall.
Tottenham imesogea mpaka nafasi ya 13 kwenye msimamo wa Ligi Kuu ikiwa na pointi 30 baada ya kucheza mechi 25 huku Man United ikishuka mpaka nafasi ya 15 ikiwa na pointi 29 ilizopata baada ya kucheza mechi 25.
Tottenham imeshinda mechi mbili mfululizo msimu huu baada ya kupata ushindi dhidi ya Brentford na Man United tangu ilipofanya hivyo tena Septemba mwaka jana dhidi ya Brentford na Man United ikiwa imezifunga mara mbili katika Ligi msimu huu.