Kipagwile, Peter waibua matumaini Dodoma Jiji

BAADA ya kukusanya pointi saba kwenye mechi tatu zilizopita, Kocha Mkuu wa Dodoma Jiji, Mecky Maxime amesema hana cha kupoteza kipindi hiki ambacho ligi inakwenda kusimama kwa takribani wiki moja huku akiwamwagia sifa washambuliaji wake kwa kuingia kwenye mfumo.

Katika mechi hizo tatu, Dodoma Jiji ilianza na sare ya mabao 2-2 dhidi ya JKT Tanzania ugenini, ikashinda 3-0 dhidi ya KenGold na 2-0 dhidi ya Kagera Sugar zote nyumbani.

Akizungumza na Mwanaspoti, Maxime amesema alianza kufanyia kazi safu ya ushambuliaji na sasa anaona kuna mabadiliko makubwa kutokana na namna wanavyotumia nafasi wanazozipata, hivyo anarudi uwanja wa mazoezi kuhangaikia safu ya ulinzi ili iwe na uwiano mzuri.

“Tunapumzika kwa kitu gani wakati hatuna uhakika wa kucheza msimu ujao licha ya kupanda hadi nafasi ya sita, wanaotufukuzia wakishinda mechi mbili na sisi tukapoteza tunateremka, hivyo kazi iliyopo ndani ya siku nane za mapumziko ni kupambania kupunguza au kuondoa makosa yaliyopo,” alisema na kuongeza:

“Tunahitaji kumaliza msimu tukiwa bora kwenye maeneo yote, sasa tumefunga mabao 29 kwenye mechi 26 tulizocheza sio wastani mzuri kwetu sawa na kuruhusu mabao tumefungwa mengi 35.

“Nafanya kazi na wachezaji ambao wamekomaa na wana uzoefu kwenye mpira, maelekezo mazuri na kukaa kama marafiki ndio kitu pekee kitaniongoza nimalize ligi nikiwa sina presha kubwa.”

Maxime alimtaja Paul Peter na Iddi Kipagwile kuwa ndio wachezaji wanaoiongoza vyema safu ya ushambuliaji ya timu hiyo huku akifurahishwa na namna wanavyopambana.

Kipagwile amefunga mabao matano na kuasisti mara mbili hivyo kahusika kwenye mabao saba huku Peter akifunga mabao manne kati ya 29 yaliyofungwa na timu hiyo.

Maxime alisema ushindani umekuwa mkubwa ingawa changamoto anayopambana nayo kwa michezo minne ijayo ni eneo la ulinzi, kutokana na mawasiliano mabovu yanayosababisha kuruhusu mabao mengi zaidi.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *