WAKATI watani wa jadi wa soka la Bongo, Simba na Yanga, wakitarajiwa kushuka dimbani katika dabi inayonadiwa kwa kaulimbiu ya HAINA KIPENGELE, kuna taarifa mbaya na ya huzuni kwa nyota wa zamani wa timu hizo mbili.
Huyu ni Mabruki Doyi Moke, kipa wa zamani wa Simba na Yanga aliyeishi kwenye mitaa ya Kariakoo kuanzia 1999 hadi 2003. Moke, raia wa DRC kutoka Bukavu ameripotiwa kuuawa asubuhi ya Machi 6, mwaka huu huko kwao Bukavu.
Sababu za kifo chake zinatajwa ni kuchomwa moto na wananchi waliojichukulia sheria mkokoni wakidhani ni mhalifu. Katika siku za hivi karibuni matukio ya wananchi kujichukulia sheria mkononi huko Bukavu nchini DRC yamekuwa mengi sana.
Sababu kubwa inatajwa kuwa ni kupambana na wimbi la uhalifu kufuatia wafungwa wote kutolewa jela na waasi wa M23 baada ya kuliteka eneo hilo. Wafungwa hao sasa wamegeuka kuwa wahalifu mitaani na wananchi hawana namna zaidi ya kuwakamata na kuwachoma moto. Kwa hiyo wananchi walimkamata Doyi Moke kimakosa wakidhani mhalifu na kumchoma moto. Hii ni habari ya kuhunisha sana.

DOYI MOKE NI NANI
Alikuja Tanzania mwaka 1997 kujiunga na timu ya Majimaji ya Songea. Mkuu wa Mkoa wa Ruvuma wa wakati ule, Anna Makinda, aliamua kuwekeza kwenye timu ili kurudisha heshima ya klabu ya Majimaji na mkoa wa Ruvuma kwa jumla.
Akamleta kocha Nzoyisaba Tauzany kutoka Burundi, na nyota wengine wengi kama akina Godfrey Kikumbizi kutoka Mtibwa Sugar, Willy Martin ‘Gari Kubwa’ kutoka Yanga, John Alex Lwena, aliyerudi Majimaji kutoka Yanga na kadhalika.
Kwa hiyo Doyi Moke alijiunga nyota hawa na kutengeneza moja ya kikosi bora na vya kuogofya miaka hiyo. Usajili wa Doyi Moke kwenda Maiimaji ulipambwa sana wakati, ikisemekana alisajiliwa kwa kiasi cha shilingi laki saba.
Kikosi hiki kikatwaa ubingwa wa Ligi Kuu ya Muungano mwaka 1998 na kushiriki klabu bingwa wa Afrika. Wakati ule ligi kuu ya Muungano ndiyo ilikuwa ligi kuu ya Tanzania na bingwa wake ndiye aliyetambuliwa na CAF na Fifa. Bingwa wa Bara alitambuliwa na CECAFA tu, na aliishia kushiriki Klabu Bingwa Afrika Mashariki na Kati (sasa Kombe la Kagame).
Mwaka 1999, Doyi Moke na wenzake wawili, Steven Mapunda ‘Garrincha’ na Amri Said ‘Stam’ wakatimkia Simba. Moke akacheza Simba hadi 2000 na kuhamia Yanga mwaka 2001 hadi 2003 alipoondoka na kutimkia Vital’O ya Burundi, timu aliyoitumikia kabla ya kuja Tanzania.

AKIWA SIMBA
Moke alifanya mengi mazuri lakini atakumbukwa zaidi kwa kashikashi aliyoipata mwaka 2000 kwenye mechi ya watani. Mechi hii iliyofanyika Agosti 5, 2000 uwanja wa taifa (sasa Uhuru), inakaribia kufanana na mechi ya safari hii. Ni kwamba siku ile Yanga ilikuwa na mchezaji mmoja aliyetoka kufunga ndoa, Idd Moshi ‘mnyamwezi’ na safari hii Yanga ina mchezaji aliyetoka kufunga ndoa, Stephanie Aziz Ki.
Katika mechi ile, bwana harusi Idd Moshi alitokea fungate moja kwa moja na kufunga mabao mawili yaliyoipa timu yake ushindi mnono wa 2-0.
Doyi Moke akiwa kwenye lango la Simba, alilaumiwa sana kwa kuihujumu timu. Yeye mwenyewe alinukuliwa akisema wakati ule kwamba sababu kuu ni kudai pesa zake hivyo anaangushiwa jumba bovu. Ushindi huo wa Yanga ulikuwa wa mwisho dhidi ya Simba, hadi Oktoba 26, 2008 kwenye mechi ya kwanza kabisa uwanja mpya wa taifa (sasa Mkapa).
Bao la mkenya Ben Mwalala likafuta uteja wa Yanga wa miaka 7 mbele ya Simba. Basi Doke akaondoka Simba baada ya msimu ule wa 2000 na kujiunga na Yanga.
Nafasi yake ikachukuliwa na Juma Kaseja, chipukizi aliyetokea Moro United akipitia Mtibwa Sugar. Naam, Kaseja alipitia Mtibwa Sugar na kucheza mechi moja tu, ya Kombe FAT, na kuondoka.
Kombe la FAT yalikuwa mashindano ya awali ya Kombe la Nyerere, likichezwa upande wa Tanzania Bara. Kombe la Nyerere ambalo lilichezwa kwa sura ya Muungano ndiyo sawa na Kombe la Shirikisho (FA) la sasa.
Basi Kaseja alicheza mechi moja tu, ya robo fainali dhidi ya Yanga na kuisaidia Mtibwa kushinda kwa matuta huku Kaseja akiokoa penati mbili za Edibily Lunyamila. Moja ndani ya dakika 90 na nyingine kwenye matuta ya mtoano.

MOKE AKIWA YANGA
Jangwani Moke atakumbukwa zaidi kutokana usajili wa kikosi chao kwenye mashindano ya Ligi ya Mabingwa Afrika. Chini ya Kocha Charles Boniface Mkwassa, Yanga ilifanya moja ya matukio yasiyotegemewa.
Walipangwa kucheza na Highlanders ya Zimbabwe (timu iliyomlea na kumkuza Prince Dube) na mechi ya kwanza Dar es Salaam iliisha kwa sare ya 2-2. Lakini wakiwa ugenini jjini Bulawayo, Yanga ilishinda 2-0 katika mechi iliyovunjika baada ya mashabiki wa Highlanders kuingia uwanjani kufanya fujo wakifomea penati ambayo Yanga walipata.
Yanga wakavuka hatua hiyo na kukutana na Mamelodi Sundowns ya Afrika Kusini. Wakapoteza 3-2 ugenini na kutoka sare ya 3-3 nyumbani, mechi iliyofanyika Mwanza. Doyi Moke alikuwa golini mechi zote hizi. Kwa hiyo ikiwa Dabi hii hii inatajwa kuwa haina kipengele, basi kipengele kiwe Doye Moke.