Paris,Ufaransa. Baada ya kuibuka shujaa kwa kuokoa michomo mingi kwenye mchezo wa hatua ya 16 bora ya Ligi ya Mabingwa dhidi ya Paris Saint-Germain, kipa wa Liverpool, Alisson Becker, amesema kiwango alichoonyesha katika mechi hiyo ni bora zaidi kuwahi kutokea katika maisha yake ya soka.
PSG walipiga mashuti 27 dhidi ya Liverpool ambao walipiga mawili tu lakini mechi ilimalizika kwa mabingwa hao wa Ufaransa kupoteza kwa bao 1-0 baada ya Harvey Elliott aliyeingia akitokea benchini kufunga sekunde 47 baada ya kuingia.
“Huu labda ulikuwa ni mchezo wangu bora zaidi katika maisha yangu ya soka. Kocha alikuwa akituambia jinsi itakavyokuwa ngumu kucheza dhidi ya PSG, jinsi wanavyokuwa bora na mpira na kwamba tungekuwa na kazi ya kuvumilia. Tulijua kilichokuwa kinakwenda kutokea,” alisema Becker.
“Tulifanya kazi kwa bidii. Juhudi zote ambazo wachezaji wenzangu walizifanya zilikuwa zinafanya kazi yangu iwe rahisi. Kisha mwishowe Harvey akaja na kufunga goli, ni hadithi nzuri kwetu. Usiku mzuri.”
Vilevile kipa wa zamani wa Manchester United, Peter Schmeichel naye alisifia kiwango cha Becker akisema ni moja ya viwango bora kuwahi kuonyeshwa na kipa kuwahi kukishuhudia.

Kocha wa majogoo hao wa Jiji la Liverpool, Arne Slot, naye alisema katika maisha yake ya ukocha Becker ndiye kipa bora zaidi kwake hadi sasa.
“Nadhani hiki ni kiwango bora cha ulinzi nilichowahi kukiona maishani mwangu. Nimefundisha wachezaji wengi wazuri kama kocha lakini kamwe sikuwahi kuona kipa bora zaidi (ya huyu) duniani hadi sasa, lakini leo alionyesha kuwa yeye ni bora duniani. Kuondoka na ushindi hapa ilikuwa zaidi ya kile tulichostahili.
“Leo tulikuwa na bahati, hiyo ni wazi kwa kila mtu. Nadhani wao walikuwa timu bora zaidi uwanjani. Hasa katika nusu ya kwanza, walikuwa na nafasi nyingi za wazi, tatu au nne.”
Mshambuliaji aliyefunga goli la ushindi, Elliott alisema: “Sina maneno, kwa kweli. Alisson, yeye ni mtu wa ajabu, kipa bora duniani. Kila mchezo anaonyesha hivyo, anatufanya tuwe na nafasi katika michezo mingi. Bila yeye, sijui tungekuwa wapi. PSG walikuwa wakipata nafasi nyingi lakini kwa mchango wa Alisson tumepata matokeo.”
Kocha wa PSG, Luis Enrique alisema Ibrahima Konate alitakiwa kutolewa kwa kadi nyekundu kutokana na makosa aliyoyafanya lakini alikiri kwamba kilichoiangusha timu yake ni kupoteza nafasi nyingi za kufunga na Liverpool itatakiwa imshukuru Becker.
Mbali ya mechi hii, pia juzi, Barcelona ilianza vizuri hatua hii ikiwa ugenini kwa kupata ushindi wa bao 1-0 mbele ya Benfica, Bayern Munich ikaichapa Bayer Leverkusen mabao 3-0 na Inter ikiwa ugenini ikaibamiza Feyenoord mabao 2-0.