Ayatullah Seyyed Ali Khamenei, Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu amehimiza kufunguliwa mashtaka maafisa wote wa kisiasa na kijeshi wa utawala wa kigaidi wa Israel kutokana na ukatili wao.
Ayatullah Khamenei alisema hayo katika chapisho lililochapishwa kwa lugha ya Kiebrania kwenye mtandao wa X, siku ya Jumamosi.
Ujumbe huo unasomeka hivi: “Makapteni wote wa kisiasa na kijeshi wa genge la kigaidi la Kizayuni lazima washtakiwe,”
Chapisho hilo limechapishwa wakati utawala wa Kizayuni wa Israel ukiendeleza mauaji ya umati dhidi ya Ukanda wa Gaza kwa zaidi ya mwaka mmoja sasa sambamba na uchokozi wa utawala huo dhidi ya Lebanon.
Tokea Oktoba mwaka jana, utawala haramu wa Israel umewaua Wapalestina wasiopungua 44,176, wengi wao wakiwa wanawake na watoto, na kujeruhi wengine 104,473 huko Gaza, huku idadi ya waliouawa huko Lebanon kutokana na mashambulizi ya utawala huo ikiwa ni zaidi ya watu 3,645, wakiwemo mamia ya watoto.

Kauli ya Ayatullah Khamenei imekuja baada ya Mahakama ya Kimataifa ya Jinai (ICC) kutoa hati za kukamatwa kwa Waziri Mkuu wa Israel Benjamin Netanyahu na waziri wa zamani wa vita wa utawala huo Yoav Gallant kuhusu jinai za kivita na jinai dhidi ya binadamu huko Gaza.
Licha ya kupongeza uamuzi huo kama “ushindi,” Iran imesema hati hizo zilipaswa kujumuisha pia “mauaji ya kimbari.”
Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Iran Esmaeil Baghaei ameandika katika ukurasa wake wa X kwamba: “Baada ya miezi 14 ya kampeni ya mauaji ya kimbari ya utawala ghasibu wa Israel huko Gaza, ambayo ilikuwa na ukatili mbaya zaidi, Mahakama ya Utangulizi ya ICC hatimaye imetoa hati ya kukamatwa kwa wahalifu wawili wakuu Netanyahu na Gallant.”
Ameongeza kuwa: “Bila shaka, mashtaka yao yalipaswa kujumuisha ‘mauaji ya kimbari’ ambayo yako wazi.”