Kiongozi wa upinzani Msumbiji atangaza masharti ya kufanya mazungumzo

Kiongozi wa upinzani Msumbiji amesema atakubali mwito wa rais wa mazungumzo baada ya ghasia kali za baada ya uchaguzi kwa masharti ikiwemo yafanyike kwa njia ya mtandao na mchakato wa kisheria dhidi yake usitishwe.

Rais Filipe Nyusi amemualika Venancio Mondlane ofisini kwake mjini Maputo Novemba 26 baada ya vifo vya watu kadhaa katika ukandamizaji wa polisi dhidi ya maandamano ya kupinga matokeo ya uchaguzi wa Oktoba 9.

Mondlane, mgombea wa kujitegemea, anayesema uchaguzi ulichakachuliwa kukipa ushindi chama cha Nyusi cha Frelimo, inaaminika aliondoka nchini kwa hofu ya kukamatwa au kushambuliwa, lakini haijulikani aliko.

Kiongozi huyo wa upinzani amesema katika hotuba aliyoitoa kwenye ukurasa wa facebook, kuwa wako tayari kwa mazungumzo ya kweli na yasiyokuwa na mitego.

Maafisa usalama wamemfungulia mashitaka kinara huyo wa upinzani, ikiwemo uharibifu uliosababishwa wakati wa maandamano ya wafuasi wake, ambayo yamepelekea akaunti zake za benki kufungiwa.

Watu wasiopungua 30 wanaripotiwa kuuawa katika maandamano ya kupinga matokeo ya uchaguzi kufuatia ushindi wa mgombea wa chama tawala cha FRELIMO Daniel Chapo. Ghasia hizo ziliikumba katika nchi hiyo ya kusini mwa Afrika baada ya uchaguzi wa rais wa Oktoba 9, ambapo Tume ya Taifa ya Uchaguzi ilitangaza kuwa, Daniel Chapo wa chama tawala cha Mozambique Liberation Front (Frelimo) ameshinda kwa asilimia 70 ya kura, lakini wapinzani wamekataa kutambua matokeo hayo.