
Kagera. Makamu Mwenyekiti wa Chama cha Wanasheria Tanganyika (TLS) Mkoa wa Kagera, Seth Niyikiza amefariki dunia akiwa kajifungia ndani mwake.
Akithibitisha tukio hilo leo Jumatano Februari 26, 2025 Kamanda wa Polisi mkoani humo, Brasius Chatanda amesema mwili wa wakili huyo ulibainika baada ya mteja wake kwenda nyumbani kwake kufuatilia kwa nini haudhurii kesi yake mahakamani.
“Alilala, hakuonekana mpaka mteja wake amekuja mahakamani hamuoni… ndio akaamua kwenda nyumbani kufika akafanikiwa kusukuma geti, kuingia eneo la ndani akakuta kuna inzi…yaani kuna ‘movement’ ya inzi nyingi kwenye dirisha hali ambayo ilimshtua ikabidi awashirikishe majirani,”amesema.
Amesema baada ya majirani kuona hali hiyo wakaamua kuvunja mlango na kumkuta amefariki na mwili umeharibika.
“Nyumba ilikuwa imefungwa mlango kwa ndani kwa tafsiri ya harakaharaka kifo kile hakina mkono wa moja kwa moja wa mtu kutoka nje kwa sababu ni kifo ambacho kwanza aliingia yeye mwenyewe, akafunga na milango yake na mule ndani hapakuwa na ‘any element of violence’ (viashiria vya ukatili) kwamba ilionekana labda kasukuma godoro…kakaa kwenye kiti chake tena kaweka na mto karelax,” amesema Chatanda.
Ameeleza kuwa pamoja na hayo wanaendelea na uchunguzi zaidi kubaini hasa kiini cha kifo chake.
Kwa mujibu wa kaka yake, Laurent Seth mwili wa marehemu umehifadhiwa katika Hospitali ya Mkoa wa Kagera mjini Bukoba, wakisubiri kufanyiwa uchunguzi ili kujua chanzo cha kifo chake.
Mkazi wa Kata Minziro Wilaya Missenyi, Egbart Rwegasira ambaye ni mtu wa karibu wa familia ya marehemu, amesema wakili huyo alikuwa ndiye msaidizi wa familia na ukoo wao kwa ujumla hivyo wamepoteza mtu muhimu.
“Msiba umeshtua sana maana ni mtu ambaye alikuwa hatumii hata vileo ila amekutwa ndani amefariki imeumiza ukoo mzima maana alikuwa anategemewa, mimi nimeanza kumfahamu muda mrefu na alikuwa wakili wangu,” amesema Rwegasira